Interpol yawatia nguvuni watu 45 magharibi mwa Afrika
30 Januari 2025Polisi ya Kimataifa, Interpol, yenye makao yake mjini Paris, Ufaransa, imesema waliokamatwa ni pamoja na mtu anayeshukiwa kuwa mwanachama wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, aliyetiwa nguvuni kwenye mpaka kati ya Mali, Niger na Burkina Faso.
Mwingine ni raia wa taifa moja la Afrika Kaskazini anayeshukiwa kuwa na dhamira ya kusafiri kupitia Ulaya kwenda kujiunga na kundi la ISIS nchini Syria.
Kwenye operesheni hiyo dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye thamani ya dola milioni 50 zilikamatwa nchini Cape Verde na aina nyingine ya dawa za kulevya zinazosisimua mwili zilikamatwa Burkina Faso.
Interpol imesema operesheni hiyo ni hatua muhimu ya kuvuruga mtandao wa uhalifu wa kupangwa unaotishia uthabiti na juhudi za kuimarisha amani na kuleta maendeleo kwenye eneo la Afrika Magharibi.