Inter yasaka ukombozi wa ligi ya mabingwa Ulaya
7 Mei 2025Kikosi cha kocha Simone Inzaghi kilikuwa katika hali tete katika wiki za hivi majuzi baada ya juhudi zao za kushinda mataji matatu kugonga mwamba na dau lao kwenda mrama kwa kupoteza uongozi wa ligi ya Seria A kwa Napoli na kutupwa nje ya Kombe la Italia na mahasimu wao wa mtaani AC Milan.
Kuishinda Barcelona iliyosheheni wachezaji nyota na kwa namna ile waliyofanya, kumeyabadili mazingira katika klabu ya Inter ambayo sasa wana fursa nziri ya kutawazwa wafalme wa soka la Ulaya kwa mara ya nne.
Inter Milan watakwaana na ima Arsenal ama Paris Saint German mjini Munich Mei 31 wakifahamu fika jukumu lao halitakuwa gumu hivyo ikilinganishwa na kibarua kigumu walichokuwa nacho miaka miwili iliyopita wakati waliposhindwa 1-0 mjini Instanbul na Manchester City iliyokuwa na kikosi bora kabisa katika enzi ya kocha Pep Guardiola. Matokeo hayo yalikuwa na uchungu mithili ya shubiri kwa Inter ambao walihisi walikuwa ndio timu bora usiku huo wa fainali.
"Tumekuwa tukitafakari kuhusu matokeo hayo tangu siku hiyo tulipoipoteza fainali," alisema nahodha Lautaro Martinez, akikaribia kutokwa na machozi ya furaha baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa Jumanne uwanjani San Siro. "Sasa tunatakiwa tupumzike na tukamilishe msimu vyema, tukifahamu tuna fursa nyingine ya kuandikisha historia."
Inter wamekuwa kila mara na sifa ya kuwa klabu ya wendawazimu inayopambana sana na yenye uwezo wa kunyang'anya ushindi mdomoni wanaposhinda mataji makubwa. Ushindi wao wa 7-6 dhidi ya Barcelona umeakisi jina lao la utani la "Pazza Inter" yaani "Inter wendawazimu".
Kocha Hansi Flick ammwagia sifa Lamine Yamal
Martinez hakuwa na uhakika wa kucheza mpaka siku moja kabla mechi lakini akapona kutokana na jeraha la mkano kwa wakati mzuri kuweza kufunga bao na kufunga penalti iliyoipa Inter uongozi wa 2-0 kufikia kipindi cha mapumziko.
Na Francesco Acerbi kwa kawaida angetokwa na damu puani mbele kwa kuwa alitakiwa kuilazimisha mechi iingine katika muda wa nyongeza kupitia bao lake la kwanza kabisa katika ligi ya mabingwa akiwa na umri wa miaka 37, wakati ilipoonekana kabisa Raphinha alikuwa amefanikiwa kuipa ushindi Barcelona baada ya kutoka nyuma.
Miamba wa Catalonia hawakuamini walichokuwa wakikiona wakati mchezaji wa akiba Davide Frattesi alipofunga bao lake la ushindi katika kipindi cha muda wa nyongeza, wakiwa hawana uzoefu wa kushindwa na kukatishwa tamaa na jinsi mchezo wao mzuri ulivyoshindwa kuzaa matunda yaliyotarajiwa.
Kocha Inzaghi ana fursa nzuri kushinda kombe la ligi ya mabingwa Ulaya
Ushindi wa Jumanne ulihisi kama nembo ya hatima ya timu kongwe ambayo imelazimika kupambana licha ya hali ngumu za kifedha na mabadiliko ya umiliki kwa jinsi kocha Inzaghi alivyoifanya Inter kuwa mojawapo ya timu mashuhuri barani Ulaya.
"Tulikuwa tunashindana na timu kubwa, lakini tumekuwa tukiuboresha mchezo wetu katika miaka minne ama mitano iliyopita, kila mwaka, na tuna fahari kubwa kwa mafanikio hayo," alisema Martinez.
Inzaghi alikuwa katika hatari ya kukamilisha msimu bila kitu isipokuwa ukosoaji na lawama baada ya kujaribu kupambana katika mashindano matatu na bajeti ndogo ikilinganishwa na vilabu vingine vikubwa vya Ulaya.
Inter, kama vilabu vingine vinavyokabiliwa na uhaba wa fedha katika ligi ya Serie A, haiwezi tena kuwavutia wachezaji nyota wa dunia kwa hiyo kocha Inzaghi amelazimika kutengeneza timu yenye ari na morali ambayo inapata matokeo katika mechi kubwa muhimu.
Ushindi mjini Munich utakuwa zawadi ya haki inayostahiki kwa kocha aliyejiunga na klabu iliyokabiliwa na msukosuko mnamo 2021 kufuatia kuondoka kwa kocha Antonio Conte na baadhi ya wachezaji nyota, na alikaribia kukabiliwa na shoka la kufutwa kazi si muda mrefu kabla Inter kutinga fainali ya ligi ya mabingwa miaka miwili iliyopita.
Uwezo wa Inzaghi ulitiliwa mashaka baada ya kupoteza mapambano ya kushinda taji la Serie A dhidi ya AC Milani katika msimu wake wa kwanza na baadaye akakamilisha msimu alama 18 nyuma ya mabingwa Napoli mnamo 2023. Lakini tangia hapo amepanda kuwa mmojawapo ya makocha wenye haiba kubwa wa soka na sasa yeye na klabu ya Inter wana fursa ya nadra maishani kushinda tuzo kubwa kabisa ya soka.