India na Urusi waendeleza biashara licha ya ushuru
21 Agosti 2025Licha ya ushuru mkubwa wa asilimia 50 uliowekwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwa bidhaa za India kutokana na hatua ya serikali ya New Delhi kununua mafuta kutoka Urusi, nchi hizo zimeonyesha dhamira ya kuendeleza mahusiano yao bila kuyumbishwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema, "Tumepata matokeo mazuri katika ushirikiano wetu kwenye sekta ya hidrojeni na kaboni, usambazaji wa mafuta ya Urusi kwenye soko la India, na tuna maslahi ya pamoja katika kutekeleza miradi ya uchimbaji wa rasilimali za nishati, ikiwemo ndani ya shirikisho la Urusi."
Marekani imeweka ushuru wa ziada wa hadi asilimia 50 kwa bidhaa kutoka India, ikiwa ni miongoni mwa viwango vya juu zaidi vya ushuru kuwahi kuwekwa na Washington.
Mataifa ya Magharibi yanayopinga mafuta ghafi kutoka Urusi yameikosoa India kwa kuendelea kununua mafuta kutoka Moscow, wakidai kuwa hatua hiyo inasaidia kufadhili vita nchini Ukraine.
Hata hivyo, India imeshikilia msimamo wake ikisisitiza kuwa uamuzi huo ni wa kibiashara tu, huku ikikosoa undumilakuwili wa mataifa ya Magharibi, ikibainisha kuwa mataifa ya Ulaya yanaendelea kufanya biashara na Moscow licha ya vikwazo.