India, China zakubaliana kuanzisha tena safari za ndege
28 Januari 2025Madola hayo mawili makubwa ya Asia yamekuwa bila uhusiano wa moja kwa moja kwa karibu miaka mitano. Safari za ndege za abiria zilisitishwa mwanzoni mwa janga la UVIKO-19. Hata hivyo, hazikuanza tena kwa sababu ya kuzorota kwa uhusiano kati ya Beijing na New Delhi.
Mvutano ulipamba moto mnamo 2020 kufuatia mapigano makali ya kijeshi kwenye mpaka unaozozaniwa huko Himalaya. Hali hiyo iliifanya India kusitisha rasmi safari za ndege za abiria kuelekea China bara.
Kulikuwa na karibu safari 500 za moja kwa moja kila mwezi kati ya China na India kabla ya janga la UVIKO-19. Uhusiano umeimarika katika miezi minne iliyopita kufuatia mikutano ya ngazi ya juu, yakiwemo mazungumzo kati ya Rais wa China Xi Jinping na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi nchini Urusi mwezi Oktoba.