IMF yashusha makaridio ya ukuaji wa uchumi wa dunia
23 Aprili 2025Mchumi mkuu wa IMF, Pierre-Olivier Gourinchas, amesema mvurugiko katika minyororo ya usambazaji duniani unaosababishwa na mashaka kuhusu ongezeko la ushuru na mvutano wa kibiashara, unaweza kuzidisha changamoto katika mazingira ya sasa ya kiuchumi.
Kauli yake imekuja baada ya IMF kuchapisha ripoti mpya kuhusu muelekeo wa kiuchumi wa duniani siku ya Jumanne, ikionesha kupungua kwa makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia hadi asilimia 2.8 kwa mwaka 2025, ikiwa ni punguzo la alama 0.5 kutoka makadirio ya mwezi Januari, na kuporomoka zaidi hadi asilimia 3.0 kwa mwaka 2026.
Kutokana na hali ya kutoeleweka kuhusu ushuru na uhusiano wa kibiashara, matatizo katika minyororo ya usambazaji yanaweza kuwa makubwa zaidi.
"Huwezi kuwa na uhakika kama wasambazaji wako bado watakuwepo, wala kama wateja wako wataendelea kununua bidhaa. Inawezekana kabisa ukalazimika kubadilisha njia nzima ya kusambaza bidhaa zako. Hii inaongeza mkanganyiko zaidi katika hali ambayo tayari ni ngumu," alisema Gourinchas.
'Pigo kwa ukuaji wa uchumi wa dunia'
Marekebisho haya ya kushuka kwa ukuaji wa uchumi yamekuja baada ya Marekani kutangaza ushuru mkubwa wa kulipiza kisasi tarehe 2 Aprili, hali iliyosababisha viwango vya ushuru duniani kufikia kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha karne moja. Ripoti hiyo inasema hali hii ni "pigo kubwa" kwa ukuaji wa uchumi wa dunia.
Nchi zilizoendelea zinakabiliwa na changamoto zaidi, na zinatarajiwa kushuhudia ukuaji wa asilimia 1.4 tu mwaka 2025 na asilimia 1.5 mwaka 2026.
Marekani imeathirika zaidi, kwani makadirio yake ya ukuaji kwa mwaka 2025 yamepunguzwa kwa alama 0.9 hadi asilimia 1.8, kutokana na hali ya kutoeleweka katika sera, mvutano mkali wa kibiashara, na kushuka kwa mahitaji ya ndani.
Chumi kubwa kuathirika zaidi
IMF inatarajia kuwa washirika wakuu wa kibiashara wa Marekani kama vile Mexico, Canada na China wote wataathirika vibaya na ushuru uliowekwa na utawala wa Trump.
China, ambayo ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani, inakadiriwa kuona ukuaji wake wa uchumi ukishuka hadi asilimia 4.0 mwaka huu, kutoka asilimia 5.0 mwaka 2024, huku ongezeko la matumizi ya serikali likishindwa kufidia athari za ushuru mpya.
Ripoti hiyo inaonya kuwa iwapo mvutano wa kibiashara utaendelea kuongezeka, ukuaji wa uchumi wa dunia unaweza kushuka zaidi na kusababisha mtikisiko mkubwa katika masoko ya fedha.
IMF inazitaka nchi kuimarisha mazungumzo, kutuliza sera za kibiashara, na kulinda uhuru wa sera za fedha ili kuimarisha uimara wa uchumi wa dunia na kuzuia hatari ambazo zinaweza kusababisha hali isioweza kudhibitika.