Idadi ya Wapalestina waliouawa Gaza yafikia 50,700
7 Aprili 2025Taarifa kutoka Ukanda wa Gaza zinasema vikosi vya Israel viliyalenga mahema yaliyofungwa nje ya hospitali mbili kubwa za ukanda huo alfajiri ya leo Jumatau na kuwaua watu wawili papo hapo akiwemo mwandishi habari.
Nje ya hospitali ya Nasser kwenye mji wa Khan Younis mahema yaliwaka moto uliosababisha kifo cha Yousef al-Faqawi, mwandishi habari wa tovuti ya habari iitwayo Palestine Today.
Mikanda ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imemwonesha mwandishi huyo akiwa anawaka moto huku mtu aliyekuwa karibu naye akijaribu kumwokoa na kuuzima.
Hata hivyo muda mfupi baadaye matabibu kwenye Ukanda wa Gaza walitangaza kwamba Yousef na mtu mwingine mmoja walipoteza maisha. Mwandishi habari mwingine aliyeshuhudia mkasa huo Abd Shaat amesimulia kilichotokea
"Mnamo saa 9 alfajiri tuliamshwa na mlio mkubwa wa mlipuko. Tukatoka nje ya mahema ndiyo tukaona hema alimokuwemo mwezetu limelengwa. Lakini sisi tutaendelea kuripoti na kutoa taarifa za ukweli kwa ulimwengu mzima. Huo ni wajibu wetu wa kibinaadamu."
Israel yasema ilikuwa inawalenga wanamgambo wa Hamas
Katika shambulizi hilo watu wengine 9 wamejeruhiwa ikiwemo waandishi habari 6. Israel ilishambulia pia mahema nje ya hospitali ya Al-Aqsa iliyopo katikati ya Gaza.
Jeshi la nchi hiyo linasema lilikuwa linawalenga wanamgambo wa Hamas lakini halijatoa maelezo zaidi. Kwa jumla tangu alfajiri ya leo watu 15 wameuawa kwenye mkururo wa hujuma za kutokea angani na ardhini zinazofanywa na vikosi vya Israel.
Hospitali ya Nasser imesema imethibitisha kupokea miili ya watu 13 ikiwemo wanawake 6 na watoto wanne.
Mashambulizi hayo yamekuwa yakiendelea kila uchao tangu utawala mjini Tel Aviv ulipotangaza kurejesha tena operesheni yake ya kijeshi ndani ya Ukanda wa Gaza baada ya kusambaratika kwa makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi Januari.
Vifo vya Wapalestina vyafikia 50,000 na Israel yadhibiti asilimia 50 ya Gaza
Ripoti ya shirika la habari la Associated Press inasema tangu kuanza awamu hiyo mpya ya mashambulizi Israel hivi sasa inadhibiti karibu asimilia 50 ya Ukanda wa Gaza.
Hali hiyo imewalazimisha mamia kwa maelfu ya Wapalestina kulundikana kwenye maeneo madogo yaliyosalia ambako hakuna kitisho cha kijeshi.
Israel inasema udhibiti huo ni wa muda mfupi na unahitajika ili kuongeza mbinyo kwa kundi la Hamas. Yenyewe inalitaka kundi hilo kuwaachilia huru mateka iliowachukua wakati wa shambulizi lake kutisha la dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7 mwaka 2023 lililowauawa watu 1,200.
Israel ilijibu shambulizi hilo kwa kuanzisha vita dhidi ya kundi la Hamas ambavyo hadi sasa vimewaua Wapalestina 50,700, takwimu zinazotolewa na mamlaka za Gaza zilizo chini ya Hamas.
Netanyahu awasili Washington kwa mazungumzo na Trump
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yuko nchini Marekani kwa mazungumzo na Rais Donald Trump. Hiyo ni ziara ya pili ya Netanyahu nchini Marekani tangu kuapishwa kwa Trump kwenye Januari.
Inafuatie ile aloifanya mwezi Februari ambapo Trump aliitumia kuutangaza mpango wake wa kuwahamisha watu wote wa Gaza na Marekani kuchukua udhibiti wa ardhi hiyo.
Mpango huo ulipingwa vikali kimataifa. Ajenda kamili ya ziara ya sasa ya Netanyahu haijafahamika, lakini inafanyika baada ya Trump kutangaza ushuru kwa bidhaa kutoka nje ambapo Israel imewekewa ushuru wa asilimia 17.