Waliouwawa katika maandamano ya Nepal wafikia 19
8 Septemba 2025Waandamanaji wanaitaka serikali kuondoa marufuku iliyowekwa kwa mitandao ya kijamii na kukomesha ufisadi. Msemaji wa polisi mjini Kathmandu, Shekhar Khanal, amethibitisha vifo hivyo.
Polisi ilijaribu kuwadhibiti maelfu kwa maelfu ya waandamanaji hao wa Gen Z, kwa kutumia risasi za mpira, maji mazito na marungu, wakati waandamanaji walipojaribu kuvunja uzio wa polisi kutaka kuelekea bungeni.
Ranjana Nepal afisa mmoja wa habari katika hospitali ya mjini Kathmandu amesema mabonu ya kutoa machozi yalirushwa pia hospitalini na kutatiza huduma za madaktari.
Mitandao mengi ya kijamii ikiwa ni pamoja na Facebook, YouTube, na X, imefungwa tangu siku ya Ijumaa wiki iliyopita baada ya serikali kufungia mitandao ya kijamii 26 ambayo haijasajiliwa, hatua iliyowachanganya na kuwakasirisha watumiaji.