Idadi ya waliouawa kaskazini-kati mwa Nigeria yafikia 150
17 Juni 2025Idadi ya watu waliofariki kutokana na shambulio lililofanywa na watu waliojihami kwa silaha mwishoni mwa juma kaskazini-kati mwa Nigeria imeongezeka hadi kufikia 150.
Watu walionusurika wameeleza kwamba washambuliaji walivamia jamii ya Yelewata katika jimbo la Benue usiku wa kuamkia Ijumaa na kuwafyatulia risasi wanakijiji waliokuwa wamelala na kuchoma nyumba zao.Wapiganaji wa itikadi kali wawauwa wakulima 14 Nigeria
Watu wengi waliouawa walikuwa wamejihifadhi katika soko la ndani baada ya kukimbia ghasia katika maeneo mengine ya jimbo.
Wanakijiji wameendelea kuchimbua nyumba zilizoteketea, wakihesabu watu waliofariki na pia kutafuta makumi ya watu ambao bado hawajapatikana.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na mauaji hayo mara moja, lakini mashambulizi kama hayo ni ya kawaida katika eneo la kaskazini mwa Nigeria ambapo wafugaji na wakulima wa eneo hilo mara nyingi hugombana kuhusu upatikanaji mdogo wa ardhi na maji.