Vifo vyapindukia 2,500 Myanmar baada ya tetemeko la ardhi
1 Aprili 2025Kwa mujibu wa kiongozi wa kijeshi nchini Myanmar, Min Aung amesema kwamba kufuatia mkasa huo zaidi ya watu 4,500 wamejeruhiwa huku wengine takriban 440 hawajulikano walipo na matumaini ya kuwapata wakiwa hai ni hafifu.
Juhudi za uokoaji bado zinaendelea na mapema siku ya Jumanne, vikosi vya uokoaji vilimuokoa mwanamke mwenye umri wa miaka 63 kutoka kwenye vifusi, huku matumaini zaidi ya kuwapata manusura wengine yakiendelea kupungua baada ya saa 72 za uokoaji.
Tetemeko hilo la ardhi lililotokea siku ya Ijumaa likiwa na ukubwa wa kipimo cha 7.7 likiathiri zaidi katika miji ya Sagaing na Mandalay ambao ni wa pili kwa ukubwa.
Soma pia:Myanmar yatangaza wiki nzima ya kuwakumbuka walioangamia kutokana na tetemeko la ardhi
Maeneo mengi ya nchi yaliyoathirika na tetemeko hilo yameachwa katika hali mbaya ikiwemo uharibifu wa miundombinu ikiwemo umeme, barabara na madaraja.
Huduma za kiutu zimeendelea kuzorota huku mashirika ya kimataifa yakiingilia kati kufanikisha huduma muhimu ikiwemo chakula, dawa na maji safi kwa waathirika wa tetemeko hilo.
Uhaba wa huduma muhimu baada ya tetemeko la ardhi
Mashirika kadhaa ya kimataifa ya misaada ya kiutu yanaripoti juu ya ukosefu mkubwa wa maji safi, madawa na makaazi baada ya tetemeko ambalo limesababisha hasara kubwa ya miundombinu muhimu ikiwemo vifo zaidi ya 2,700.
Marcoluigi Corsi, Mratibu wa Misaada wa OCHA nchini Myanmar, amewaambia waandishi wa habari kwa njia ya video kwamba kuna uhaba mkubwa wa mahitaji muhimu ikiwemo maji na makazi kwa waathirika.
"Muda wa uokoaji wa dharura unapungua, hakuna mahema, maji safi wala dawa." alisema.
Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yameelezea wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa mahitaji ya msingi ikiwemo maji safi na uwezekano wa kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
"Hali si nzuri, kwa sasa hitaji kubwa ni maji, hali ya hewa ni joto kali.. Mabomba na matanki ya maji taka yameharibika." Alisema Julia Rees, Naibu Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
Soma pia:Tetemeko jengine laupiga mji wa Mandalay, Myanmar
Kwa upande wake Shirika la Afya Duniani WHO limeripoti juu ya hospitali kuzidiwa na wagonjwa huku dawa zikikaribia kuisha, wakati shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi la UNHCR likielezea hali hiyo ni kama janga kubwa la kibinadamu.
Changamoto ya kufikishwa misaada
Tayari misaada ya dharura kwa awamu ya kwanza ikiwemo mahema, blankenti ya kujifunika na vyandarua kwa ajili ya kujikinga na mbu, ikipelekwa kwa waathirika.
Hata hivyo juhudi za kufikisha misaada katika maeneo yaliyoathirika zinakwamishwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu, na hatari ya vilipuzi vilivyotegwa ardhini kutokana na vita vya miaka minne iliyopita.
Soma pia:Waliokufa Myanmar kutokana na tetemeko wafikia zaidi ya 1000
Myanmar imekuwa katika hali ya machafuko tangu mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021, ambapo jeshi liliiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia iliyoongozwa na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi.
Machafuko hayo yamesababisha uasi wa silaha dhidi ya jeshi, na kuwalazimu zaidi ya watu milioni 3.5 kuyakimbia makazi yao.