ICC kusikiliza kesi dhidi ya mbabe wa kivita, Joseph Kony
8 Septemba 2025Majaji wa mahakama hiyo hapo kesho Jumanne (09.09.2025) watasikiliza keshi 39 za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu dhidi ya Kony, yakiwemo mauaji, mateso na ubakaji. Kesi hiyo itasikilizwa bila ya mshukiwa huyo kuwepo mahakamani.
Kony, mwenye umri wa miaka 63, amekuwa akisakwa na mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini The Hague tangu mwaka 2005. Anasakwa kwa tuhuma hizo kufuatia miongo mitatu ya ukatili wa kundi lake la waasi wa Lord's Resistance Army, LRA, katika mataifa kadhaa ya Kiafrika.
Kony alianzisha uasi katika miaka ya 1980 dhidi ya utawala wa Rais Yoweri Museveni, ambao ulisambaa hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan. LRA inatuhumiwa kuwauwa zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 waliolazimishwa kuwa watumwa wa kingono na askari.