Huenda Iran wamefariki zaidi ya watu 20,000.
28 Desemba 2003TEHERAN: Siku mbili baada ya kutokea balaa kubwa la mtetemeko wa ardhi huko Iran kungali bado hakuna uhakika kuhusu kiwango cha watu waliouawa. Waziri wa Mambo ya Ndani Abdulwahed Mussawi-Lari alisema mjini Teheran huenda wameuawa zaidi ya watu 20,000. Alikuwa akisahihisha takwimu nyingine zilizotangazwa rasmi kwamba wameuawa kasoro ya kiwango hicho. Tayari zimekwisha zikwa maiti 15,000, alisema Bwana Mussawi, kwa mujibu wa taarifa ya Televisheni ya Iran. Katika mji wa Bam ulioteketezwa karibu wote, makundi ya kuokoa maisha yanaendelea kuwatafuta watu ambao huenda wamenusurika chini ya vifusi vya majumba yaliyoteketezwa. Shirika rasmi la Habari la Iran, IRNA limearifu Jumamosi ya jana na Jumapili ya leo wameweza kuokolewa watu wapatao 10,000 walionusurika. Mbali na makundi ya Kiiran, makundi ya kuokoa maisha kutoka nchi 21 yanafanya kazi kutwa kucha katika maeneo yaliyoteketezwa. Tayari zimekwisha wasili ndege 45 kuleta vifaa vya misaada kutoka nchi za nje.