HRW yasema mzozo wa nchini Kongo unaweza kuwa 'janga'
26 Januari 2025Mtafiti mkuu wa shirika la HRW barani Afrika, Clementine de Montjoye, amesema hali inayowakabili raia wa Goma inazidi kuwa ya hatari na mahitaji ya kibinadamu ni makubwa. Kwenye taarifa yake shirika hilo limetahadharisha kuhusu matokeo mabaya yatakayowafika watu katika eneo hilo la mashariki mwa Kongo.
Soma Pia: Kongo: Kundi la M23 laua watu watano huko Masisi
Kwa upande wake Umoja wa Afrika umehimiza "kusitishwa mara moja" kwa mapigano makali mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ametoa wito wa kukomeshwa kwa uhasama na amezitaka pande zinazohusika kuhakikisha usalama wa raia.
Kauli hiyo imetolewa wakati ambapo vikosi vya M23 vinavyoungwa mkono na Rwanda vinapambana na vikosi vya walinda amani wa kigeni pamoja na jeshi la Kongo.
Jumla ya walinda amani tisa wa Afrika ya Kusini wameuwawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati walipokuwa wakipambana na waasi wa kundi la M23. Wizara ya ulinzi ya Afrika ya Kusini imethibitisha vifo hivyo vya wanajeshi wake hao.
Soma Pia: Wakazi wakimbia wakati waasi wa M23 wakiusogelea zaidi mji wa Goma
Taarifa ya wizara hiyo ya ulinzi ya Afrika Kusini, imefafanua kuwa, walinda amani saba kati ya waliouwawa kufikia siku Ijumaa walikuwa sehemu ya jeshi la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, na wawili walikuwa wanatoka kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Kongo MONUSCO.
Wakati huo huo jeshi la Uruguay pia limetangaza kuwa, mwanajeshi wake mmoja aliyekuwa katika Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameuwawa, na wenzake watano wamejeruhiwa.
Takriban walinda amani 15,000 wa Umoja wa Mataifa wako nchini Kongo.
Wakati huo huo msemaji wa jeshi la Malawi Emmanuel Mlelemba, pia amethibitisha kuuawa wanajeshi watatu wa Malawi waliokuwa sehemu ya jeshi la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC katika mapambano na waasi wa kundi la M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma Pia: Watu 55 wameuwawa mashariki mwa DRC
Rais wa Angola Joao Lourenco amezitaka Rwanda na nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kurejea kwenye mazungumzo ya amani, ambayo yalivunjika mwaka jana.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya kikao cha dharura siku ya Jumapili kujadili hali ya nchini Kongo baada ya Kinshasa kuwaondoa wanadiplomasia wake kutoka nchini Rwanda. Na Rwanda kwa upande wake imewaamuru wanadiplomasia wake kurejea nyumbani kutoka nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mapigano makali kati ya wanajeshi wa Kongo na wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda hadi kufikia siku ya Jumapili yalifika karibu na mji wa Goma ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu kaskazini katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Chanzo: AFP