HRW: Wanamgambo wamewaua zaidi ya watu 127 Niger
10 Septemba 2025Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti leo inayoonyesha kwamba kundi la wanamgambo wanaohusishwa na kundi la kiislam lenye itikadi kali la Islamic State wamezidisha mashambulizi magharibi mwa nchi ya Niger na kuua zaidi ya watu 127 katika mashambulizi tofauti tangu mwezi Machi mwaka huu.
Ripoti hiyo iliangazia hali ya kiutu katika maeneo ya ukanda wa Sahel ambayo mara kwa mara yamekabiliwa na mashambulizi ya wanamgambo ikiwemo katika mkoa wa Tillaberi, karibu na mpaka na Burkina Faso na Mali.
Eneo hilo la mpakani linajulikana kama kitovu cha shughuli za wanamgambo hao wa kijihadi huko Afrika Magharibi na ambao pia wanatajwa kuwa na ushirikiano na makundi ya kiislam ya itikadi kali yaIslamic State na al-Qaeda.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kwamba mashuhuda wameeleza kuwa jeshi la Niger halijafanya vya kutosha kukabiliana na mashambulizi hayo na kupuuza maombi ya wanakijiji juu ya wasiwasi wao kiusalama. Niger haijatoa tamko lolote juu ya ripoti hiyo.