HRW:Serikali ifanikishe haki za waandamanaji waliouawa Kenya
27 Juni 2025Kadhalika inapaswa kutekeleza kanuni za kimataifa na kuhakikisha katika siku zijazo, utendaji wa vikosi vya usalama kwa maandamano yanayoendelea nchini humo ni halali na unazingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Maelfu ya watu waliingia barabarani Asubuhi ya Juni 25 jijini Nairobina katika kaunti kadhaa za Kenya katika kumbukumbu ya vifo vya waandamanaji waliouawa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano ya Juni 2024. Ripoti za awali za vyombo vya habari zilionyesha kuwa, pamoja na kuwepo kwa polisi, serikali ya Kenya ilipeleka wanajeshi kukabiliana na idadi kubwa ya waandamanaji waliokuwa wakielekea katika maeneo ya kibiashara ya Nairobi na Ikulu, makazi rasmi ya rais.
Watu 16 wauawa na zaidi ya 400 wamejeruhiwa Kenya
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, takriban watu 16 waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, akiwemo mmoja katika kaunti za Machakos, Kisii na Nakuru, huku zaidi ya watu 400 wakiripotiwa kulazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta wakiwa na majeraha ya risasi na majeraha mengine. Miongoni mwa waliolazwa kwa matibabu ni mwanahabari wa NTV Ruth Sarmwei, ambaye alipigwa na risasi ya mpira alipokuwa akiripoti maandamano hayo.
Otsieno Namwaya ambae ni mkurugenzi mshiriki wa Afrika katika Human Rights Watch anasema "Mambo ya kutumia risasi wakati wa maandamano yanafaa yakome, pili kuna mauaji ya kiholela ambayo yamefanyika mwaka huu, mwaka jana na ule mwaka mwingine wa 2023. Hatujaona uchunguzi ukifanyika vizuru. Uchunguzi unapaswa kufanyika na wale waliohusika wachuliwe hatua."
Human Rights Watch yalaani Kenya kutumia jeshi dhidi ya waandamanaji
Aidha Namwaya pia amekemea kitendo cha mamlaka ya Kenya kutumia jeshi katika kukabiliana na raia." Kila nchi inasheria zake lakini jeshi linafaahamika kimataifa ni la kulinda nchi kwa vitisho vya nje. Ndani ya nchi ni kazi ya pilisi inafaa kutumika, kwa hivyo tuna wasiwasi kwanini serikali ya Kenya ikaamua kutumia jeshi. Kwa kawaida waandamanaji hawabebi silaha, ni jambo ambalo halifahi kuhusishwa jeshi, linafaa kushughulikiwa na polisi." Alisema afisa huyo mwandamizi waHRW.
Jana Alhamis Umoja wa Mataifa ulisema "umesikitishwa sana" na ghasia wakati wa maandamano nchini Kenya na kuhimiza utulivu pamoja na kufanyika uchunguzi huru kufuatia athari za maandamano hayo.
Mamlaka ya Kenya yatangaza msako mkali kwa waliovuruga biashara
Aidha Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Kipchumba Murkomen alitathmini uharibifu wa biashara katika mji mkuu, Nairobi, ambapo bidhaa ziliibiwa katika maduka mengi na kuwaahidi wamiliki wa maduka hayo kwamba polisi watafuatilia kamera zao za usalama - CCTV na kuwatia mbaroni wahusika.
Soma zaidi:Waziri Kipchumba Murkomen asema maandamano ya Jumatano yalikuwa ugaidi
Mapema Jumatano katika kaunti 23 kati ya 47 za taifa hilo walifanya maandamano ya kushinikiza kukomeshwa kwa ukatili wa polisi na kuhimiza utawala bora. Katika maandamano maelfu waliimba kauli mbiu ya kumtaka Rais William Ruto kujiuzulu. Kimsingi waandamanaji wengi walighadhibishwa na kifo cha hivi karibuni cha mwanablogu kilichoteka mikononi mwa polisi sawia na tukio lingine la kupigwa risasi kwa raia wakati wa maandamano ya kupinga kifo cha mwanablogu.