Hotuba ya Rais Bush, Brussels,Ubelegiji
21 Februari 2005Brussels:
Rais George W. Bush wa Marekani, akiwa katika ziara yake ya nchi za Ulaya, leo amezungumzia masuala kadhaa ya kimataifa katika hotuba yake muhimu aliyoitoa mjini Brussels, Ubelegiji. Katika hotuba yake ametoa mwito wa kuboreshwa kwa uhusiano uliopo kati ya Marekani na nchi za Ulaya na hasa baada ya kumalizika kwa vita vya Irak. Amesema kwamba mvutano uliosababishwa na vita hivyo sasa unapaswa kuzikwa na kipaumbele kiwe amani ya Mashariki ya Kati. Kuhusu Iran amesisitiza kwamba lazima nchi hiyo iache kuunga mkono ugaidi na azma yake ya kutengeneza silaha za kinuklia. Ameonya kwamba haondoi uwezekano wa kutumia nguvu dhidi ya nchi hiyo. Rais Bush amezipongeza Israeli na Palestina kwa kuonyesha nia ya kufungua ukurasa mpya katika kutafuta amani ya Mashariki ya Kati. Kuhusu Siria amesema kwamba lazima nchi hiyo iondoe majeshi yake nchini Lebanon kwani inamkandamiza jirani yake. Wakati huo huo, ametoa mwongozo wake kuhusu majukumu ya siku zijazo ya Shirika la Kujihami la Magharibi (NATO). Rais wa Marekani atakutana na Kansela Gerhard Schröder wa Ujerumani siku ya Jumatano mjini Mainz.