Hofu yaongezeka Ukingo wa Magharibi kugeuka Gaza ya pili
14 Februari 2025Katika lango la kuingia kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walitazama kwa tahadhari huku magari ya kijeshi ya Israel na ambulensi za Kipalestina zikipita. Wengine walikuwa wakiondoka, nyuso zao zikiwa zimechoka, wakiwa na mizigo yao michache mikononi.
Ala'a Aboushi, mkazi wa eneo hilo, alikuwa akiwagawia waandishi wa habari vikombe vidogo vya kahawa ya Kiarabu. "Wameimaliza Gaza, na sasa wamekuja hapa kwetu Ukingo wa Magharibi kutulipiza kisasi," aliIambia DW. "Kama raia, hatujisikii salama hata kidogo."
Mnamo Januari 21, mara baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa Kipalestina katika Jenin, eneo linalochukuliwa na Israel kuwa ngome ya wapiganaji hao.
Tangu wakati huo, mashambulizi hayo yameenea hadi miji mingine kama Tulkarem, jiji lingine kubwa Kaskazini Magharibi mwa Ukingo wa Magharibi. Jiji hilo lina kambi mbili za wakimbizi, Tulkarem na Nur Shams, zilizojengwa baada ya kuundwa kwa Israel mwaka 1948 ili kuhifadhi Wapalestina waliopoteza makazi yao.
Mashambulizi mapya yanasababisha uharibifu zaidi
Eneo hili lina historia ndefu ya mashambulizi ya kijeshi ya Israel. Tangu shambulizi la Hamas Kusini mwa Israel Oktoba 7, 2023, uvamizi wa jeshi la Israel umekuwa ukiongezeka kwa ukubwa na ukali. Operesheni ya hivi karibuni imetokea wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa akiingia rasmi madarakani, huku akisema atatoa tamko hivi karibuni kuhusu mpango wa Israel wa kulinyakua kabisa eneo la Ukingo wa Magharibi.
Soma pia: Jeshi la Israel lalipua majengo kadhaa Jenin
Mashambulizi haya mapya yamehusisha mashambulizi ya anga na uvamizi wa ardhini, yakiambatana na uharibifu wa miundombinu, ubomoaji wa nyumba, kufukuzwa kwa watu kwa nguvu, vifo na kukamatwa kwa watu. Watu wengi wanahofia kuwa Ukingo wa Magharibi unaweza kuwa Gaza ya pili.
"Jeshi la Israel linashirikiana kwa nguvu katika kambi ya wakimbizi ya Jenin ili kuwamaliza magaidi na kuharibu miundombinu yao, kama tulivyoona leo," alisema Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, Januari 29. "Kambi ya wakimbizi ya Jenin haitarudi tena kama ilivyokuwa. Baada ya operesheni hii, vikosi vya IDF vitabaki katika kambi hiyo kuhakikisha ugaidi haurudi tena."
Tamko hili lilitolewa baada ya vikosi vya usalama vya Palestina kuendesha operesheni yao dhidi ya wapiganaji wa Palestina katika kambi hiyo. Mamlaka ya Palestina ina udhibiti mdogo sana katika baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi. Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya wakimbizi 40,000 wa Kipalestina wamelazimika kuyahama makazi yao kwa nguvu.
Tangu mashambulizi ya Israel yaanze, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UN OCHA) inaripoti kuwa angalau Wapalestina 39 wameuawa, wakiwemo 25 huko Jenin, 10 Tubas na 4 Tulkarem, miongoni mwao wakiwa wapiganaji na raia, akiwemo mwanamke mjamzito wa miaka 23 na mtoto mdogo.
Kwa upande wake, vyombo vya habari vya Israel vinaripoti kuwa vikosi vya IDF vimewaua zaidi ya wapiganaji 60 wa Kipalestina na kuwakamata zaidi ya 210 tangu operesheni ianze.
Kila uvamizi unazidi kuwa mbaya zaidi
Umm Mohammed, mkazi wa kambi ya wakimbizi ya Tulkarem, amesema kuwa ameona uvamizi mwingi wa kijeshi maishani mwake, lakini kila mmoja unakuwa mkali zaidi. "Kila wakati unakuwa mbaya zaidi kuliko uliopita. Tulikuwa tunalia kwa hofu na wasiwasi." Alisema risasi zilikuwa zikifyatuliwa ovyoovyo kila mahali, na baada ya siku chache waliwambiwa waondoke kwenye nyumba zao.
Tangu wakati huo, Umm Mohammed, watoto wake na wajukuu wake wamekuwa wakiishi kwenye chumba kidogo katika klabu ya michezo ya ndani, ambayo imewapa hifadhi wakimbizi waliokimbia mashambulizi. Mchango wa nguo na blanketi kutoka kwa watu binafsi umejazana mlangoni. Runinga iliyopo ndani inaonyesha matangazo ya moja kwa moja kutoka nyumbani – kambi za wakimbizi za Tulkarem na Nur Shams. Watoto wanajaribu kujifunza mtandaoni kwa sababu shule nyingi zinazohudumiwa na Umoja wa Mataifa zimefungwa.
Soma pia: Machozi na shangwe kwa Wapalestina walioachiwa Ukingo wa Magharibi
Mwanawe Umm Mohammed, Ahmed, alisema anakataa madai ya Israel kwamba inawalenga tu wapiganaji. "Nikikuwa nyumbani kwangu, ninapaswa kujisikia salama. Wewe unakuja kama mwanajeshi mvamizi na kunifukuza nje. Kwa haki gani? Kuna mtu mwenye silaha hapa?" alisema, akiongeza kuwa hata haruhusiwi kuondoka kambini akiwa kwenye kiti chake cha magurudumu ya umeme na sasa anategemea msaada wa wengine.
Lakini hata kuondoka kambini ni tatizo, kwani barabara nyingi zimeharibiwa vibaya, familia yake ilisema. Katika mji wa Jenin, jeshi la Israel lililipua majengo karibu 20 upande wa mashariki wa kambi hiyo, likidai kuwa yalikuwa na vifaa vya kijasusi vya wapiganaji na maabara za kutengeneza mabomu. Kwa wengi waliopo hapa, uharibifu huu unawakumbusha jinsi Gaza ilivyoteketezwa baada ya vita.
Mustakabali usiojulikana
Mashambulizi haya mapya pia yameambatana na vizuizi katika vituo vya ukaguzi vya kijeshi vya Israel katika Ukingo wa Magharibi, hali ambayo imevuruga maisha ya wakazi wake wapatao milioni 3. Jeshi la Israel lilithibitisha kwa DW kuwa "kwa mujibu wa maagizo ya uongozi wa kisiasa, imeamuliwa kubadili utaratibu na kupanua ukaguzi kwenye vituo vya ukaguzi vya Ukingo wa Magharibi."
Mjini Tulkarem, ambapo barabara nyingi zinazoelekea mjini humo zimefungwa na wanajeshi wa Israel, Umm Mohammed alisema huwa anaangalia habari kila siku, akisubiri kwa hamu kuruhusiwa kurudi nyumbani. Lakini pia anahofia kuhusu wanyama wao vipenzi – paka watano na ndege wadogo kadhaa – waliolazimika kuwaacha nyuma. "Tulibakiza chakula kwao, lakini sasa ni zaidi ya wiki moja. Ninaogopa tutawakuta wote wamekufa tutakaporudi."
Kwa kuwa mtaa wao umeondolewa wakaazi wake, hakuna aliyebaki kuwahudumia, na hakuna anayejua hali hii itaendelea kwa muda gani.