Hofu mjini Gaza baada ya Israel kuwaagiza wakaazi kuhama
9 Septemba 2025Agizo hilo limetolewa baada ya Israel kutoa onyo kali kwamba itapanua oparesheni zake za kijeshi kwa kile walichokiita "kimbunga kikuu" ikiwa kundi la Hamas halitawaachilia mateka wa mwisho walioko mikononi mwao.
Wakaazi wa mji huo, wapatao takriban milioni moja, wamekuwa wakihofia mashambulizi kwa wiki kadhaa, tangu Israel ilipotangaza mpango wa kuliangamiza kabisa kundi la Hamas katika ngome zao za mwisho.
Agizo hilo la kuhama limezua hofu na taharuki kubwa miongoni mwa wakaazi wa mjio huo. Baadhi yao wamesema hawana budi ila kuelekea maeneo ya kusini mwa Gaza huku wengine wakisisitiza kwamba watabaki mjini humo kwa sababu hakuna sehemu nyingine salama ya kukimbilia.
Wakaazi wa Gaza tayari wamehamishwa mara kadhaa tangu vita vilipoanza mnamo Oktoba mwaka 2023, wakihama kati ya maeneo ya kaskazini na kusini mwa ukanda huo wa pwani, hali ambayo imezidisha janga la kibinadamu na kusababisha baa la njaa inayozidi kuathiri maisha ya maelfu ya Wapalestina.