Hofu ya kufutika kwa makubaliano ya kupatikana amani Juba
9 Machi 2025Makubaliano dhaifu ya kugawana madaraka kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar yako hatarini kuvunjika kufuatia mapigano kati ya vikosi vyao hasimu katika jimbo la Upper Nile nchini humo.
Mnamo siku ya Ijumaa, helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa ikijaribu kuwaokoa wanajeshi katika jimbo hilo ilishambuliwa, na kusababisha kifo cha mmoja wa wafanyikazi wa helikopta hiyo na kuwajeruhi watu wengine wawili.
Soma pia: Wanasiasa watatu wa Sudan Kusini wakamatwa
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS ulieleza Ijumaa kuwa, jenerali mmoja wa jeshi pia aliuawa katika jaribio la uokoaji lililoshindikana.
Tukio hilo lilizua hofu katika taifa hilo changa na maskini, ambalo kwa muda mrefu limekumbwa na misukosuko ya kisiasa na ghasia. Kiir, mnamo Ijumaa usiku, alitoa wito wa utulivu na kuahidi kwamba hawatarejea tena vitani.
Wito watolewa kwa viongozi kuheshimu haki za binadamu
Katika taarifa yake ya Jumamosi, mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Yasmin Sooka alieleza kuwa, nchi hiyo inashuhudia kile alichokiita "kurudi nyuma kwa maendeleo ya kupatikana amani, hali ambayo inatishia kufuta juhudi za miaka mingi ya kutafuta suluhu."
Amesema, "badala ya kuchochea mgawanyiko na migogoro, viongozi wanapaswa kuzingatia haraka mchakato wa amani, kuheshimu haki za binadamu za raia wa Sudan Kusini na kuhakikisha mchakato mzuri wa mpito kuelekea demokrasia."
Sudan Kusini, nchi changa zaidi duniani, ilimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitango mnamo mwaka 2018 kupitia makubaliano ya kugawana madaraka kati ya mahasimu wakuu Salva Kiir na Riek Machar.
Soma pia: Machar: Mkataba wa amani Sudan Kusini uko hatarini
Hata hivyo, washirika wa Kiir wamemtuhumu Machar na vikosi vyake kwa kuchochea vurugu katika eneo la Nasir, jimbo la Upper Nile kwa kushirikiana na kundi linalojulikana kama White Army, kundi la vijana wenye silaha kutoka jamii ya Nuer, ambayo ni jamii anayotokea Makamu wa Rais.
Mwanzoni mwa mwezi wa Machi, vikosi tiifu kwa Rais Salva Kiir viliwakamata mawaziri wawili na maafisa kadhaa wa ngazi ya juu wa jeshi ambao ni washirika wa Riek Machar.
Msemaji wa serikali Michael Makuei ameeleza kuwa, watu hao walikamatwa kwa sababu washirika hao wa Machar wamevunja sheria. Amevishtumu vikosi vinavyomtii Machar kwa kushirikiana na jeshi la White Army na kushambulia kambi ya kijeshi karibu na mji wa Nasir mnamo Machi 4.
Chama cha Machar hata hivyo kimekanusha tuhuma hizo.
"Tunachoshuhudia sasa ni kurejea kwa makabiliano ya kuwania madaraka ambayo yaliiharibu nchi hapo awali," amesema Kamishna Barney Afako katika taarifa ya Tume ya Umoja wa Mataifa.
Ameongeza kuwa raia wa Sudan Kusini wamevumilia ukatili, ukiukaji wa haki za binadamu unaofikia viwango vya uhalifu mkubwa, usimamizi mbaya wa uchumi, na hali ya usalama inayozidi kuzorota.
"Wanastahili kupumzika na kupata amani, sio kuingia tena kwenye mzunguko mwingine wa vita."
Umoja wa Afrika AU pia umeelezea wasiwasi wake, ukitoa taarifa siku ya Jumamosi na kulaani vikali ongezeko la ghasia na kuhimiza usitishwaji mara moja wa uhasama nchini humo.