Hofu ya vita Ulaya yazua wimbi la uandikishaji jeshini
24 Agosti 2025Shule ya sheria haikumfundisha Constance jinsi ya kufanya mazoezi, kutambua alama za mawasiliano ya redio, au kulala kifudifudi juu ya zege huku akielekeza bunduki yake kwa adui. Badala yake, mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Sorbonne alipata mafunzo yake ya kijeshi kutoka kwa kikosi kilichoko katika mji mkuu wa Paris, wakati wa likizo ya kiangazi.
"Nadhani ni muhimu sana kulilinda taifa letu, hasa katika muktadha wa sasa", alisema mwanafunzi huyo wa mwaka wa pili wa sheria kuhusu mafunzo yake ya wiki mbili ya kujiunga na jeshi la akiba. Kwa ombi la jeshi la Ufaransa, jina lake la mwisho na ya wengine waliotajwa katika taarifa hii hayajachapishwa.
"Nadhani jeshi ndilo njia bora ya kujifunza jinsi ya kufanya kazi kwa ushirikiano," aliongeza.
Zaidi ya miongo miwili baada ya Ufaransa kusitisha mafunzo ya kijeshi ya lazima, maelfu ya Wafaransa sasa wanaomba kujiunga na jeshi la akiba, wakitumai kupata nafasi ya kulitumikia taifa lao, hata kwa muda mfupi. Idadi ya wanajeshi wa akiba wanaofanya kazi imeongezeka kwa kasi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kutoka 28,000 mwaka 2014 hadi zaidi ya 46,000 hivi sasa. Jeshi la nchi kavu limechukua zaidi ya nusu yao, huku waliobaki wakigawanyika kati ya jeshi la majini na jeshi la anga.
Macron aongeza uwekezaji wa kijeshi
Ifikapo mwaka 2035, serikali inalenga kuongeza zaidi ya mara mbili idadi ya wanajeshi wa akiba — hadi kufikia 105,000, sawa na mmoja kwa kila wanajeshi wawili wa kawaida — na kutoa fursa mpya kwa vijana kujitolea. Lengo hilo linaendana na mpango wa Rais Emmanuel Macron wa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika jeshi, hadi kufikia euro bilioni 64 ($75 bilioni) mwaka 2027, ikiwa ni mara mbili ya kiwango cha mwaka 2017 alipoingia madarakani.
Muktadha wa ongezeko hilo, sambamba na juhudi kama hizo barani Ulaya, ni hofu inayoongezeka kuhusu Urusi inayozidi kuwa na msimamo mkali — pamoja na mashaka ikiwa Marekani chini ya Rais Donald Trump itaitetea Ulaya ipasavyo.
"Kamwe...uhuru wetu haujawahi kutishiwa kiasi hiki", Macron alisema katika hotuba ya televisheni mwezi Julai. "Tunahitaji kuharakisha juhudi za kuimarisha akiba yetu ya kijeshi. Tunahitaji kuwapa vijana mfumo mpya wa kulitumikia taifa."
Afisa mkuu mstaafu katika jeshi la Ufaransa, Patrick Chevallereau, aliuita msukumo wa Macron kuwa "hatua nzuri" — ingawa alionya kuwa bajeti ya serikali kwa ujumla bado inapaswa kupitishwa na Bunge la Ufaransa.
"Sio tu kwamba tunahitaji watu wengi zaidi," aliongeza Chevallereau, ambaye sasa ni mchambuzi wa Taasisi ya Huduma za Ulinzi ya Royal United yenye makao yake mjini London, "bali tunahitaji watu waliobobea zaidi katika maeneo muhimu" kama vile matumizi ya droni na teknolojia ya habari.
Mafunzo makali huko Versailles
Jukumu la kuwafundisha wanajeshi wapya wa akiba limekabidhiwa kwa Kikosi cha 24 cha Wapiganaji huko Versailles, kilichoko katika eneo kubwa la kijeshi takriban kilomita nne kutoka kasri maarufu la mji huo.
"Wengine wanataka kugundua ulimwengu wa kijeshi na kuona kama wanataka kujiunga kwa muda wote," alisema Luteni Amelie, aliyesimamia kikao cha mafunzo cha hivi karibuni. "Wengine huja kwa sababu ya changamoto ya kuzoea mazingira tofauti, au kwa sababu ni kuchelewa kujiunga na jeshi la kawaida."
Kama wanachama wengi wa Kikosi cha 24 cha Wapiganaji, Amelie naye ni mwanajeshi wa akiba; katika maisha yake ya kiraia, anafanya kazi kama afisa wa forodha. Alitumia majira ya kiangazi kusimamia mafunzo makali ya wiki mbili kuhusu maisha ya kijeshi.
Wakiwa na umri kati ya miaka 17 hadi 57, wakufunzi wake 51 walitumia siku ndefu za mafunzo, wakiamka saa 12 asubuhi na mara nyingi wakilala saa sita usiku.
"Wanajifunza kutumia na kubeba silaha zao kwa usalama, kuandamana kwa pamoja, kutumia dira na vifaa vya mawasiliano," alisema Amelie kuhusu wakufunzi hao, akiorodhesha baadhi ya mahitaji ya mafunzo hayo ya awali. "Tunafanyia kazi mbinu zote za mapigano zinazotumiwa na kikosi chetu."
Katika asubuhi moja ya hivi karibuni, kikundi hicho kilifanya mazoezi huku wakiimba kwa mpangilio, wakajifunza kutumia bunduki zao, na baadaye wakafanya mazoezi ya kufyetua risasi.
"Mafunzo haya ni magumu sana," alisema Constance, mwanafunzi wa sheria, ambaye aliongeza kuwa anawajua wanafunzi wengine wa Chuo Kikuu cha Sorbonne waliopitia mafunzo hayo pia. "Hatuna umri sawa, kazi sawa, wala masomo sawa, lakini tunajifunza jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja."
Kama Constance, Gabriel ambaye ni mhandisi mwenye umri wa miaka 23, aliomba kujiunga na jeshi la akiba kwa sababu anahofia mustakabali wa nchi yake. "Kama mwanajeshi, sitatoa maoni kuhusu masuala ya kisiasa au kiitikadi," alisema, akieleza msimamo wa wanajeshi wengine wa akiba waliokataa kujadili waziwazi tishio la Urusi. "Lakini vita iko mpakani mwa Ulaya, na ni ishara kwetu kuchukua hatua."
Onyo jingine la tahadhari kwa mhandisi huyo kijana lilikuwa shambulio la kigaidi la Bataclan mwaka 2015 huko Paris.
"Kuna kitu kilibadilika ndani yangu," alisema Gabriel. "Nilitambua kuwa kipindi cha amani nilichokijua na kukulia kimekwisha. Na nikafikiri, 'Nitajitokeza na kutoa mchango wangu."
Juhudi za kuongeza idadi ya wanajeshi zinaendelea pia katika sehemu nyingine za Ulaya, huku nchi hizo zikijaribu kujibu changamoto za kiusalama zinazoongezeka. Ripoti ya awali mwaka huu kutoka kwa vituo vya tafiti vya Bruegel na Kiel Institute ya Ujerumani ilikadiria kuwa Ulaya inaweza kuhitaji wanajeshi 300,000 wa ziada kwa muda mfupi ili kuzuia uchokozi wa Urusi, bila msaada wa Marekani.
Nchi zaidi Barani Ulaya zachukua hatua
Baadhi ya nchi tayari zimechukua hatua. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Lithuania, Sweden na Latvia zimeanzisha tena mafunzo ya kijeshi ya lazima. Poland imetangaza mipango ya kutoa mafunzo ya kijeshi kwa raia 100,000 kila mwaka. Ujerumani nayo iko katika harakati za kuajiri wanajeshi wapya, na — kutokana na mwitikio wa awali kuwa mdogo — Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius ameonya kuwa huduma ya lazima jeshini inaweza kurejeshwa endapo watu wachache watajitolea.
Nchini Ufaransa, hali ni tofauti — tafiti zinaonyesha kuwa kuna uungwaji mkono mkubwa kwa juhudi za kukuza jeshi. Utafiti wa IPSOS-CESI uliofanywa mapema mwaka huu ulionyesha kuwa asilimia 86 ya Wafaransa wanaunga mkono huduma ya kijeshi, zaidi ya nusu waliidhinisha huduma ya lazima. Utafiti mwingine uligundua kuwa nusu ya vijana wa Kifaransa wako tayari kujiunga na jeshi endapo vita vitatokea.
"Nadhani watu wanaelewa kuwa huenda wakalazimika kulinda kile wanachokithamini," alisema mchambuzi wa masuala ya ulinzi Chevallereau. "Kuongezeka kwa jeshi la akiba kunaweza kuwa njia ya kuimarisha uhusiano kati ya kizazi kipya na jeshi."
Kikosi cha 24 cha Versailles, kilichoanzishwa katika karne ya 17, kimesema kinapokea wimbi la maombi ya kushiriki mafunzo yake. Kwa kila waombaji 100, ni 40 tu wanaochaguliwa. Wanaohitimu wanaweza hatimaye kutumia hadi siku 60 au zaidi kwa mwaka wakihudumu katika akiba. Malipo kwa mwanajeshi wa akiba ni ya wastani — kati ya €40 hadi €200 kwa siku, kulingana na cheo.
Sio kila mtu anayekamilisha hata mafunzo ya awali. Kati ya watu 61 waliochaguliwa kwa kikao cha hivi karibuni cha Kikosi cha 24, 10 walijiondoa. "Wengine walijiondoa mwanzoni mwa mafunzo kwa sababu hawakuwa na muda," alisema mkufunzi Amelie. "Wengine walitambua kuwa siyo mambo yao, mara tu waliposhika silaha mikononi mwao."
Baada ya kuhitimu, kikundi chake kitafanya mafunzo ya ziada kwa miezi kadhaa. Mara watakapokubalika kuwa tayari, wengi wao huenda wakajiunga na doria za kitaifa chini ya Operesheni Sentinelle — operesheni ya usalama iliyoanzishwa baada ya mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 2015 nchini Ufaransa — na ambayo ilitoa ulinzi wakati wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka jana. Wale wenye ujuzi maalum wanaweza pia kutumwa nje ya nchi.
Bertrand, baba wa watoto wawili, amesaini mkataba wa kuhudumu kwa miaka mitano katika jeshi la akiba baada ya kumaliza mafunzo yake. Akiwa na umri wa miaka 30, alikumbuka jinsi alivyopata habari kuhusu mashambulizi ya mwaka 2001 kwenye Kituo cha Biashara cha Dunia huko New York.
"Tumepitia mashambulizi mabaya pia hapa Ufaransa," alisema. "Nilihisi ni wajibu wangu kama baba kulitetea taifa langu." Akiwa mfanyakazi wa halmashauri katika mji nje ya Paris, Bertrand anaamini kuwa tayari anahudumia taifa lake kama raia. "Sasa nitakuwa nalihudumia taifa langu kama mpiganaji," alihitimisha.
(Ripoti ya Elisabeth Bryant)