Hiroshima yaadhimisha miaka 80 tangu kupigwa kwa bomu
6 Agosti 2025Mji wa Hiroshima nchini Japan leo siku ya Jumatano umewakumbuka wahanga wa shambulio la bomu la atomiki lililotokea miaka 80 iliyopita.
Jiji la Hiroshima lilinyamaa kimya ilipowadia saa 8:15 asubuhi, muda huo ndio bomu lilipodondoshwa mnamo Agosti 6, mwaka 1945. Joto na mionzi kutokana mlipuko wa bomu hilo uliliharibu kabisa jiji la Hiroshima na watu 140,000 walikufa.
Manusura wengi ambao sasa wana umri mkubwa wa zaidi ya miaka 86, wameelezea kufadhaika kwao juu ya viongozi wa kimataifa wanaonekana kuunga mkono matumizi ya silaha za nyuklia.
Mmoja wa manusura ni Minoru Suzuto, mwenye umri wa miaka 94, anasema pengine kwa wazee wengi kama yeye, kumbukumbu ya leo huenda ikawa ya mwisho na kwamba hakutakuwa na mtu wa kulielezea tukio hili la kusikitisha na la uchungu katika miaka 10 au 20 ijayo.
Bomu la pili liliangushwa siku tatu baadaye katika mji wa Nagasaki ambako watu 70,000 walikufa. Japan ilijisalimisha mnamo Agosti 15, na kuhitimisha Vita vya Pili vya Dunia na uvamizi wa taifa hilo wa karibu nusu karne kwenye bara la Asia.
Meya wa Hiroshima Kazumi Matsui ametahadharisha juu ya kuongezeka vituo vya kijeshi na kupendekeza matumizi ya silaha za nyuklia kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa kwa kuzingatia vita vya Urusi huko nchini Ukraine na mizozo katika eneo la Mashariki ya Kati. Marekani na Urusi ndio nchi zinazoamiliki sehemu kubwa ya makombora ya nyuklia duniani.
Meya Kazumi amekitaka kizazi cha vijana kiendeleze mapambano ya kupinga matumizi ya silaha za nyuklia.
Takriban watu elfu 55 wamehudhuria sherehe za mwaka huu. Meya wa Hiroshima Matsui alibandika orodha iliyorekebishwa ya watu waliofariki kwenye eneo la kumbukumbu ya watu waliokufa katika vita. Orodha hiyo mpya sasa ina majina 349,246 ikiwa ni pamoja na majina ya wahanga 4,940 ambao vifo vyao vilithibitishwa katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba Shigeru pia amezungumza kwenye hafla hiyo. Amesema Japan imejitolea kuhakikisha kuwa ulimwengu unatokomeza silaha za nyuklia.
Vyanzo: DPA/AP