HILLA:Hujuma za waasi zaongezeka Iraq kuelekea kura ya maoni juu ya katiba
30 Septemba 2005Mripuko wa bomu la ndani ya gari uliofanyika ndani ya soko lililokuwa limejaa watu umewauwa takriban watu 11 na kuwajeruhi wengine 30 hii leo mjini Hilla.
Shambulio hilo limetokea siku moja baada ya watu zaidi ya 60 kuwawa kwenye mripuko wa bomu la kutegwa ndani ya gari kaskazini mwa Baghdad mjini Balad.
Waasi wanendeleza hujuma zao nchini humo kujaribu kuiondoa madarakani serikali inayoungwa mkono na Marekani.
Kura ya maoni ikikaribia juu ya katiba mpya ya Iraq kumeongezeka wasiwasi wa kuzuka vita vya kimadhebu kati ya washia waliowengi na wasunni waliowachache nchini Iraq.
Katika wiki za hivi karibuni waasi wamekuwa wakiendeleza hujuma zao kwa kasi mno licha ya Marekani kudai kwamba wamewaweza wale wanaowaita magaidi na wapiganaji wa kigeni wanaoendeleza umwagikaji damu nchini Iraq.