Hezbollah yasema haitaki vita na Israel
1 Aprili 2025Ammar ameyatoa matamshi hayo Jumanne kusini mwa Beirut, karibu na eneo ambako Israel imefanya mashambuliuzi ya anga na kuwaua takriban watu wanne na kuwajeruhi wengine wapatao saba.
Amesema kundi la Hezbollah limekuwa na ''uvumilivu wa hali ya juu'', lakini ameonya kuwa uvumilivu huo una mipaka yake. ''Hatutaki vita na Israel. Ngoja tuwe wazi, Hezbollah haitaki vita. Lakini wakati huo huo, kama vita vitaanzishwa juu yetu, Hezbollah iko katika tahadhari ya juu kuzuia uchokozi wowote ule,'' alisisitiza Ammar
Israel yathibitisha kumuua afisa wa Hezbollah
Jeshi la Israel, IDF limethibitisha kumuua Hassan Ali Mahmoud Bdeir, afisa wa Hezbollah na kamanda wa kikosi maalum cha Iran cha Quds, katika shambulizi la usiku kwenye viunga vya mji wa Beirut, katika eneo la Dahieh.
IDF imesema katika taarifa yake kwamba shambulizi la sasa lilimlenga kamanda wa Hezbollah, ambaye amekuwa akilisaidia kundi la Kipalestina la Hamas katika Ukanda wa Gaza dhidi ya mashambulizi ya Israel. Kulinga na Israel, shambulizi hilo limefanyika kwa maelekezo ya Shirika la Ujasusi la Israel, Shin Bet.
Aidha, shambulizi hilo limefanyika bila kuwepo tahadhari, siku chache baada ya Israel kuanzisha shambulizi kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut, siku ya Ijumaa, likiwa ni shambulizi la kwanza tangu yalipomalizika makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah yaliyofikiwa mwezi Novemba.
Lebanon yalaani mashambulizi
Rais wa Lebanon, Joseph Aoun amelaani vikali shambulizi hilo la anga, na amewatolea wito washirika wa Lebanon, kuunga mkono ''haki ya utawala kamili'' wa nchi yake. Aoun amesema ukiukaji wote wa uhuru lazima uzuiwe.
Naye Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam amelitaja shambulizi hilo kama ''ukiukaji wa wazi'' wa makubaliano ya kusitisha mapigano ya November 25 yaliyomaliza mapigano ya zaidi ya mwaka mmoja kati ya Israel na Hezbollah. Baadhi wa wabunge wamesema serikali inapaswa kuhakikisha usalama wa Walebanon.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametengua uteuzi wa mkuu mpya wa ujasusi wa nchi hiyo, muda mfupi baada ya kumteua. Netanyahu amemshukuru Eli Sharvit, kamanda wa zamani wa jeshi la wanamaji, kwa nia yake ya kuchukua majukumu hayo, wakati wa mkutano wao.
Ofisi ya Netanyahu imesema Jumanne kuwa, kiongozi huyo alimuarifu Sharvit baada ya kutafakari kwa kina, kwamba anataka kuwaangalia wagombea wengine. Hata hivyo, hakuna sababu zozote zilizotolewa kuhusu utenguzi huo.
Soma zaidi: Netanyahu amteua mkuu mpya wa shirika la ujasusi
Siku ya Jumatatu, ofisi ya Netanyahu ilitangaza kuwa Sharvit atachukua nafasi ya Ronen Bar kuwa Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Israel.
Ama kwa upande mwingine, wizara ya afya inayoongozwa na Hamas huko Gaza, imesema kuwa watu 1,042 wameuawa katika eneo la Palestina, tangu Israel ilipoanzisha tena mashambulizi makubwa ya anga, Machi 18.
(DPA, AFP, AP, Reuters)