Hemedti wa RSF aapishwa kuiongoza serikali sambamba ya Sudan
31 Agosti 2025Hatua hiyo inaashiria kugawanyika kwa taifa hilo katikati ya vita vya miezi 28 kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha RSF kinachoongozwa na mbabe huyo wa kivita. Wakati jeshi likidhibiti maeneo ya kati na mashariki, RSF inadhibiti sehemu kubwa ya Darfur na imekuwa ikipambana kudhibiti mji wa kihistoria wa al-Fasher, ambako mamia ya maelfu ya raia wamezingirwa kwa zaidi ya siku 500, wakilazimika kula chakula cha mifugo ili kuishi.
Mashirika ya kimataifa ya hisani kama vile UNICEF na Yale Humanitarian Lab yameripoti vifo vya mamia ya watoto na vizuizi vya raia kuondoka, huku wengine wakieleza kushambuliwa na kuporwa. Vita hivyo vimesababisha njaa kwa nusu ya wananchi, kudhoofisha uchumi, na kuibua janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani, huku juhudi za Marekani kumaliza mzozo huo zikikwama.