Havard yakataa masharti ya Rais Trump
17 Aprili 2025Upande mmoja ni Chuo Kikuu cha Harvard, chuo kikuu kongwe na tajiri zaidi Marekani, kinachojulikana kwa hadhi kubwa. Upande mwingine ni utawala wa Trump, unaopania kubadilisha kwa kiasi kikubwa mfumo wa elimu ya juu.
Mgogoro huu unaweza kujaribu mipaka ya mamlaka ya serikali na uhuru wa vyuo vikuu vya Marekani, ambao umevifanya kuwa kivutio kwa wasomi duniani.
Havard yakataa hadharani masharti ya serikali
Kwa mara ya kwanza, Harvard imeamua kukataa hadharani masharti ya serikali yanayolenga kuzuia maandamano ya wanafunzi yanayounga mkono Palestina na kuachana na sera zinazofatia utofauti na ujumuishaji, hatua iliyochochea serikali kuzuwia ruzuku na mikataba yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni mbili.
Kukatizwa kwa ufadhili kunaweza kuwa na madhara makubwa
Mwandishi wa Assocated Press Cllin Binkley, anasema hatua inaweza kuwa na madhara makubwa.
Binkley amesema Harvardimepinga hadharani masharti ya utawala wa Trump kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi vyuoni, jambo lililopelekea serikali kuzuwia zaidi ya dola bilioni mbili za ufadhili.
Ameongeza kuwa hatua hiyo huenda ikazua mvutano wa kisheria kuhusu mipaka ya mamlaka ya serikali na uhuru wa taasisi za elimu.
Harvard inasema fedha hizo hufadhili tafiti muhimu za kitabibu.
Havard yawaajiri wanasheria mashuhuri kupambana na Trump
Tayari chuo cha Harvard kimewaajiri wanasheria mashuhuri na wenye uhusiano na Trump na watu wake wa karibu kuendesha mchakato wake wa kisheria dhidi ya Trump, ikiapa kuwa haitasalimu amri linapokuja suala la uhuru wake wa kitaaluma na utafiti.
Havard imetakiwa kumomba Rais Trump msamaha
Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, anasema Rais Trump anataka Harvard iombe radhi kwa kile anachokiita chuki dhidi ya Wayahudi kwenye chuo hicho.
Leavitt anadai kuwa uongozi wa Harvard ulifeli kuwachukulia hatua wanafunzi walioendesha maandamano na kusababisha usumbufu wa masomo chuoni.
Havard yasema masharti ya serikali ya Trump yanakiuka katiba
Harvard kwa upande wake imesema masharti hayo yanakiuka katiba na uhuru wa kujieleza, ikisisitiza kuwa chuo hakiwezi kuruhusu serikali kuchukua udhibiti wa kitaasisi.
Mvutano huu sasa unaelezwa kuwa kipimo cha jinsi serikali ya Marekani inaweza kutumia nguvu dhidi ya taasisi za elimu kupitia udhibiti wa ufadhili.
Vyuo vingine vyaiunga mkono Havard
Tayari vyuo vingine kama Columbia, Stanford na Princeton vimeonesha kuunga mkono msimamo wa Harvard.
Wachambuzi wanasema hii huenda ikageuka kuwa mapambano mapya ya kisheria kuhusu haki za kikatiba, uhuru wa kitaaluma, na mipaka ya mamlaka ya serikali kwa taasisi binafsi.
Ni wazi kuwa mvutano huu kati ya Harvard na serikali ya Trump unaweza kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa elimu ya juu Marekani.