Hatma ya makada wa CHADEMA waliojiondoa yazua mjadala pana
8 Mei 2025Siku moja baada ya makada watano wa ngazi za juu ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania kutangaza kujiondoa, gumzo limeibuka kuhusu hatma yao ya kisiasa huku wanasiasa, wachambuzi na wanazuoni wakitafakari iwapo ni anguko kwa chama au fursa mpya kwa vyama vingine.
Waliotangaza uamuzi huo ni pamoja na Bara Benson Kigaila, Salum Mwalimu, Catherine Ruge, John Mrema na Julius Mwita — wote wakiwa wajumbe wa zamani wa sekretarieti ya chama hicho. Wameeleza kuwa CHADEMA kimepoteza mwelekeo na kwamba chama hicho kinaendeshwa kwa mtindo wa kiharakati badala ya kisera.
Hata hivyo, makada hao wamesisitiza kuwa hawatajiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakisema kufanya hivyo ni kuwasaliti wananchi waliowaamini kuwa wapinzani wa kweli. "Hatuhamii CCM kwa sababu ni chama kilicho madarakani. Sisi tunabaki kuwa sauti mbadala ya wananchi,” amesema John Mrema.
Kuhusu uwezekano wa kuanzisha chama kipya, Mrema amesema hilo halitawezekana kwa sasa kwa sababu muda wa usajili umekwisha, lakini nia yao ni kuendelea na siasa kwa kuwania nafasi kama ubunge, udiwani au hata urais.
Hawahamii CCM, hawasajili chama kipya — lakini wanapanga kurudi kwenye siasa. Vipi?
Tayari vyama kadhaa vya siasa vimeonekana kuwa na hamu ya kuwapokea, ingawa bado hawajafanya uamuzi rasmi kuhusu wapi wataelekea. "Tunapokea maombi mengi lakini bado tunatafakari kwa kina,” amesema Mrema.
Soma pia: Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kusikilizwa mahakama ya wazi
Kwa upande wa wachambuzi wa siasa, maoni yamegawanyika. Profesa Albert Kinyondo anaona hatua hiyo kama anguko la kisiasa kwa makada hao, akisema huenda hawataweza kujijenga tena kisiasa nje ya CHADEMA.
Lakini mchambuzi mwingine, William Kasembe, anasema uamuzi huo unaweza kuibua chachu ya mageuzi ya kweli ya upinzani nchini, ikiwa makada hao wataungana kwa dhima mpya inayowakilisha wananchi kwa karibu.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa na makada hao kuondoka ni pamoja na kutengwa ndani ya chama mara baada ya kuonyesha kuunga mkono msimamo wa Mwenyekiti wa zamani Freeman Mbowe, hali iliyozua migawanyiko ya wazi ndani ya CHADEMA.
Je, makada hawa wanakwenda wapi? Hili ndilo swali linaloendelea kulitikisa jukwaa la siasa Tanzania. Wakati wakichukua muda kufikiria hatua yao inayofuata, taswira ya upinzani nchini huenda ikabadilika kwa kiasi kikubwa miezi ijayo.