Hatma ya kocha Ancelotti kujulikana mwisho wa msimu
19 Aprili 2025Kocha wa klabu ya Real Madrid nchini UhispaniaCarlo Ancelottiamesema leo kwamba hatima yake ndani ya klabu hiyo itaamuliwa baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi kuu La Liga mwishoni mwa mwezi Mei.
Kocha huyo raia wa Italia na ambaye amekuwa akihusishwa na timu ya taifa ya Brazil, aliulizwa juu ya mustakabali wake na waandishi wa habari hii leo kabla ya mechi yao ya ligi dhidi ya Athletic Club kesho Jumapili.
Soma zaidi: Arsenal na Inter zatinga nusu fainali Champions League
Katikati mwa wiki, Real Madrid ilitupwa nje na Arsenal katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya katika hatua ya robo fainali na baada ya hapo tetesi zilianza kuibuka kwamba kocha huyo huenda akabwaga manyaga baada ya mchezo ujao wa fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya Barcelona mnamo Aprili 26.
Ancelotti mwenye umri wa miaka 65 ndiye kocha pekee aliyewahi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano, mara tatu akiwa na Real Madrid na mara mbili akiwa na AC Milan ya Italia.