Hatma ya waziri mkuu Bayrou yaning'inia bungeni
8 Septemba 2025Nchini Ufaransa, Waziri Mkuu Francois Bayrou anakabiliwa na kitisho cha kuangushwa kupitia kura ya maoni itakayopigwa muda wowote kutoka sasa katika bunge la nchi hiyo. Ufaransa iko kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi.
Bayrou,ambaye hatma ya uongozi wake inaning'inia kwenye kamba inayoshikiliwa na bunge la Ufaransa, amewaomba wabunge kumuunga mkono kwenye mapendekezo yake ya bajeti na kupunguza deni la nchi hiyo.
'' Endapo tungekuwa na kiwango sawa cha uzalishaji kama majirani zetu, Ufaransa isingekuwa na tatizo la nakisi wala deni. Uzalishaji kwahivyo ni suala la dharura kwa taifa''
Muda mfupi uliopita Bayrou mwenye umri wa miaka 74 ameyazungumza hayo bunge katika kile ambacho kimetajwa kama juhudi zake za mwisho za kujaribu kutetea nafasi yake, akiwaambia wabunge kwamba madeni yanakaribia kabisa kuizamisha Ufaransa na kutishia mustakabali wa Umoja wa Ulaya.
Hata hivyo wabunge na hasa wa upinzani ambao baadae watapiga kura ya imani , inatajwa kwamba huenda wakumuondowa madarakani.
Ufaransa ina hali mbaya ya kifedha
Deni la umma nchini humo limeongezeka hadi asilimia 113.9 la pato la ndani huku takwimu zikionesha kwamba nakisi ya mwaka jana ilipindukia karibu mara mbili ya asilimia 3 ya kiwango cha mwisho kilichowekwa na Umoja wa Ulaya.
Kutokana na hali hiyo mbaya ya kiuchumi, waziri mkuu huyo ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa siasa za wastani za mrengo wa kulia,ambaye ni waziri mkuu wa nne tangu rais Macron kurudi tena madarakani,aliamuwa kutangaza bajeti yake ya mwaka 2026 ambayo itaihitaji Ufaransa itafute njia ya kuokoa yuro bilioni 44.
Lakini hiki hasa ndicho kilichowakasirisha wapinzani ambao sasa wanasema hakuna njia nyingine isipokuwa kumtimuwa bwana Bayrou. Gabrielle Cathala ni mbunge asiyeyumbishwa nchini Ufaransa.
"Nafurahi sana na hii kura ya maoni.Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano, tuna haki ya kuwa na kipindi hiki cha kuendesha demokrasia katika bunge letu la taifa . Tumejaribu kumzuia bwana Bayrou mara nane. Na mara hizo nane aliokolewa na bibi Le Pen na mara sita na Wasoshalisti. Hatimae sasa, jioni hii demokrasia ya bunge itapata fursa ya kuonekana''
Kura ya imani aliyoiitisha Bayrou ni kujitia kitanzi?
Waziri mkuu Bayrou aliitisha kura ya imani bungeni kuhusu mpango wake huo wa kiuchumi, hatua ambayo inaonesha wazi kwamba ni mchezo wa bahati nasi, utakaoamuliwa na upinzani ambao tayari umeiita hatua hiyo kama ni ya kujitowa muhanga kisiasa.
Kishindo cha kura ya imani bungeni kinazidi kuitumbukiza Ufaransa katika mkwamo wa kisiasa na kiuchumi kipindi ambacho Ulaya iko katika wakati mgumu ikitafuta mshikamano mbele ya macho ya Urusi ambayo inapigana na Ukraine lakini pia kuongezeka kwa ushawishi wa China na mivutano ya kibiashara na Marekani.
Nchi hiyo inakabiliwa na shinikizo kubwa la kuitaka irekebishe hali yake ya kifedha na hasa kutokana na nakisi kubwa iliyoshuhudiwa mwaka jana.
Mpaka sasa rais Macron amekataa kulivunja bunge na endapo Bayrou atapoteza kura hii ya imani bungeni bila shaka rais Macron atalazimika kutafuta waziri mkuu mpya atakayeweza kusimamia bajeti kupitishwa bungeni ikiwa ni chini ya mwaka mmoja baada ya kutimuliwa mtangulizi wa Byrou,Michel Barnier.