Imani za itikadi kali zaenezwa magerezani, Kongo
8 Julai 2025Ukosefu wa mafunzo kwa maafisa wa magereza, uangalizi mdogo na kuwachanganya wafungwa wa kiraia na wale kutoka makundi ya waasi vinachangia pakubwa kuzidisha tatizo hilo.
Tukiangazia pekee hali ilivyo katika gereza la Beni huko Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC , ushuhuda kutoka kwa wafungwa wa zamani unaonyesha kuwa wafungwa huhamasishana kuwa na misimamo mikali inayoweza kupelekea hadi kwenye ugaidi. Vitendo hivyo huendeshwa na wafungwa wenye mafungamano na waasi wa ADF. Hali inayoibua wasiwasi mkubwa katika gereza hilo la Beni, ni kwamba raia wa kawaida huzuiliwa pamoja na wapiganaji wa makundi yenye silaha.
Mfungwa tuliempa jina Gustave ambalo si jina lake halisi alizuiliwa kwa muda wa miezi minane katika Gereza la Kangbayi huko Beni kati ya mwaka 2021 na 2022. Anasema alishuhudia wafungwa wenzake wakihamasishwa kuwa na itikadi kali na kwamba hiyo imekuwa kama desturi gerezani hapo.
Gustave anasema watu hao huwahadaa wafungwa kwamba washirika wao wana mpango wa kuvamia gereza hilo na kuwaokoa wanachama wake pekee, jambo linalopelekea wafungwa hao kuwa na matumaini. Itakumbukwa kuwa mnamo Oktoba 20, 2020, gereza la Beni lilishambuliwa na mamlaka zilieleza kuwa angalau wafungwa 1,300 walitoroka. Kundi la kigaidi la IS huko Afrika ya Kati lilidai kuhusika na tukio hilo.
Mazingira yanayochochea kuenea kwa itikadi kali
Kulingana na Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO), takriban watu 400 kutoka makundi kadhaa yenye silaha, ikiwa ni pamoja na ADF, waasi wa AFC/M23 na hata askari na polisi waliofanya uhalifu wanazuiliwa katika gereza hilo la Beni. Jean Tobi Okala wa Afisa Habari wa MONUSCO huko Beni anaamini kuwa mchanganyiko huo kichocheo cha kueneza imani za itikadi kali.
"Gereza hili linawahifadhi watu mbalimbali. Kuna raia, wanachama wa makundi yenye silaha, polisi na askari wa zamani. Pia iko katikati ya eneo lenye vita. Mchanganyiko huu unapelekea watu kuwa na itikadi kali. Kwa hiyo, baada ya kuondoka gerezani, watu hawa huwa hatari zaidi kuliko walipoingia."
Mateso ya wafungwa na kukosa faraja vinachangia pia
Mwandishi wa habari za uchunguzi Nicaise Kibel'Bel Oka ambaye ameripoti mno kuhusu kundi la kigaidi la ADF lenye mafungamano tangu mwaka 2017 na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu (IS), anasema wanamgambo wa makundi yenye silaha hutumia fursa ya kuwahamisha imani za itikadi kali wafungwa wa kiraia kutokana na hali ya mateso walionayo gerezani wakijaribu kuwapa aina fulani ya "faraja ya kihisia na kiroho," akisisitiza kwamba jambo hilo limekuwa tatizo kubwa kwa kuwa wafungwa huishi katika magereza hayo bila uangalizi wowote.
" Hasa pale familia yako inapokutelekeza, unakuwa chini ya himaya ya wale wanaoweza kukupa chakula gerezani, na kwa hakika, wanaanza kukuhubiria kuhusu itikadi kali za Uislamu, wakikuahidi pepo, na ndipo unajikuta unazidi kuwa na misimamo ya itikadi kali."
Maafisa wa magereza wameelezea kufahamu changamoto hiyo na wanajaribu kuzuia tishio hilo la kuenea kwa uhamasishaji wa itikadi kali kwa kuwapa mafunzo maafisa wa magereza. Katikati ya mwezi Juni 2025, maafisa wa magereza ya Beni walipata mafunzo hayo hasa kuhusu upotoshaji na namna ya kuzuia kuenea kwa imani za itikadi kali magerezani.
(DW)