Harvard yapoteza mabilioni baada ya kugomea utawala wa Trump
15 Aprili 2025Chuo Kikuu cha Harvard kimejikuta katika mvutano mkali na serikali ya Rais Donald Trump baada ya kukataa kutekeleza masharti mapya yaliyowekwa na Wizara ya Elimu ya Marekani.
Serikali imesitisha ruzuku ya zaidi ya dola bilioni 2.2 pamoja na mikataba ya thamani ya dola milioni 60, ikitaka mabadiliko ya kina katika sera za chuo hicho kuhusu udahili na ajira kwa misingi ya utofauti, usawa na ujumuishaji.
Soma pia: Jaji asema wahamiaji wanatendewa vibaya kuliko manazi na utawala wa Trump
Barua ya serikali iliyopelekwa kwa uongozi wa Harvard ilitaka pia chuo hicho kianze kuripoti wanafunzi wa kigeni wanaokiuka kanuni kwa mamlaka, na kurekebisha vigezo vya udahili kwa wanafunzi wa kimataifa.
Hata hivyo, Rais wa Harvard, Alan Garber, amesema hatua hiyo ya serikali ni kinyume na katiba na kwamba chuo hicho hakiwezi kukubali kuachia uhuru wake wa kielimu au kufuata mashinikizo ya kisiasa.
Wizara ya Elimu imesema kauli ya Harvard inaonyesha dhana ya upendeleo wa vyuo vya hadhi ya juu kuhusu fedha za umma, na kwamba masharti hayo yanakusudia kuhakikisha haki za kiraia zinalindwa, hasa dhidi ya unyanyasaji wa wanafunzi Wayahudi.
Vyuo vingine nchini Marekani, kama Columbia, tayari vimekubali masharti hayo ili kuendelea kupokea ufadhili wa serikali.