Hamas yatathmini pendekezo jipya la kusitisha mapigano Gaza
15 Aprili 2025Viongozi wa Hamas wamesema wanatathmini kwa umakini mkubwa pendekezo la hivi sasa la kusitisha mapigano walilolipokea kutoka kwa wapatanishi na kwamba watatoa majibu yao baada ya kukamilika kwa mchakato wao wa mashauriano.
Katika taarifa, kundi la Hamas limesema kuwa makubaliano yoyote ni lazima yajumuishe usitishaji wa kudumu wa vita, kuviondoa kabisa vikosi vya Israel katika Ukanda huo, kubadilishana wafungwa, kuwepo mpango wa ujenzi mpya wa maeneo yaliyoharibiwa na vita, na kuondolewa kwa vizuizi na mzingiro wa Gaza.
Matakwa ya Israel kwa Hamas
Israel kwa upande wake inapendekeza usitishwaji mapigano kwa siku 45 ikiwa Hamas itawachilia huru nusu ya mateka waliosalia na inataka pia wanamgambo wa Hamaswapokonywe silaha, lakini kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina limesema huo ni mstari mwekundu na kueleza kuwa limewatuma wajumbe wake nchini Qatar kuendelea na mazungumzo hayo ya amani.
Kwa sasa Israel na Hamas wanashiriki mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango mpya wa usitishaji mapigano huko Gaza baada ya kushindwa kwa juhudi za kurefusha muda makubaliano ya awali. Misri, Qatar na Marekani ndio wanaendelea na jukumu hilo la upatanishi kwenye mazungumzo hayo.
Israel yaendeleza mashambulizi katika ukanda wa Gaza
Hayo yakiripotiwa, Israel imeendeleza mashambulizi huko Gaza na kusabisha vifo vya makumi ya watu.
Aidha, watu 10 wakiwemo madaktari watatu na wagonjwa saba wamejeruhiwa baada ya Israel kushambulia hivi leo hospitali moja huko Gaza. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaja kusikitishwa pia na shambulizi la Jumapili katika hospitali ya al-Ahli akisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, wahudumu wa afya, watu waliojeruhiwa na wagonjwa pamoja na vituo vya matibabu, ikiwa ni pamoja na hospitali lazima viheshimiwe na kulindwa.
Israel yashambulia hospitali kaskazini mwa Gaza
Vita vya Gaza vilianza Oktoba 7 mwaka 2023 baada ya kundi la Hamas kuvamia kusini mwa Israel na kuuwa watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 250. Mashambulizi makali ya kulipiza kisasi ya Israel tayari yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 51,000 katika ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.